Home Uncategorized KAZE SIO MALAIKA, KILA MMOJA LINAMHUSU

KAZE SIO MALAIKA, KILA MMOJA LINAMHUSU


Anaandika Saleh Jembe 

WATU hawapendi kuelezwa ukweli zaidi ya yale maneno matamu ambayo yanakuwa ni kupakana mafuta kwa kutumia mgongo wa chupa.


Ukweli unajenga na ukweli unafundisha lakini ukweli unakumbusha kwenda katika uhalisia.


Leo ninaendelea huku nikianza kukupa pole kama utaumia kwa kuwa utaendelea siku nyingine na ndiyo kazi yangu. Leo nawakumbusha, Kocha Cedric Kaze raia wa Burundi ambaye tayari amesaini kuanza kuinoa Yanga, si malaika.


Nimeona baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao walikwenda kumpokea Kaze wakati akitua wakionyesha matumaini makubwa sana ya mabadiliko wakiwa na imani na kocha huyo.


Hili ni sahihi kabisa, tunafundishwa kuishi kwa matumaini badala ya kutomuamini kila mmoja na hii haiwezi kuwa sawasawa kama itatokea kuna jambo limeshindwa kufanyika unaangalia upande mwingine wa kuelekeza matumaini ili kuendelea kusonga mbele.


Wakati Kaze akielekezewa matumaini hayo, lazima kuwe na imani ya uvumilivu pia kwa kuamini kuna wakati Kaze kama mwanadamu naye atakutana na ugumu ambao kuuvuka kunahitajika uvumilivu kutoka pande zote.


Hapa ninazungumzia kwanza kabisa upande wa mashabiki ambao kwa kuwa wana matumaini makubwa na ikatokea kidogo mambo hayajabadilika haraka sana kama walivyotarajia, basi wanaweza kumpa muda fulani kocha huyo.


Ukiangalia timu zote kubwa mbili za kwao Burundi alizozifundisha Kaze ni ndogo, angalau Atletico. Timu kubwa na kongwe kwa Burundi ni Vital’O na Inter Stars, lakini nazo haziwezi kuwa na presha kubwa kama ya Yanga au kubwa kama ya Ligi Kuu Bara.


Kaze amefundisha hadi timu za vijana za Barcelona, lakini unajua bado hakuna presha kubwa sana kama ambayo utakutana nayo katika klabu kubwa na kongwe yenye mashabiki wengi kama Yanga.


Kwa sasa mashabiki wako katika ushindani mkubwa na uchovu wa kuona Simba wanaendelea kuchukua ubingwa mfululizo kwa mara ya tatu. Hamu hii lazima inakuwa na msukumo na inaweza kuwafanya mashabiki kulalamika kwa kila jambo lakini lazima wakubali, mabadiliko atakayoanza kuyafanya Kaze katika kikosi chake haliwezi kuwa jambo la siku moja.

SOMA NA HII  SIMBA YASHUSHA BOMU, YANGA KUMEKUCHA, KESHO NDANI YA CHAMPIONI JUMAMOSI


Katika mpira mambo ni tofauti kidogo, si kila kitu kinaweza kufanikiwa mara moja, muda ni lazima. Hivyo hata kama ikitokea Kaze ameanza na ushindi, aina ya uchezaji, uingizaji wa mifumo kufikia kiwango anachokitaka, muda utatakiwa.


Wakati mwingine timu chini yake inaweza kupoteza na hii inakuwa ni sehemu ya yeye kwenda kupata kile anachotaka. Kama kweli anaaminika, lazima avumiliwe kwa kuwa yeye si malaika, ni kocha kama makocha wengine ana anachokuwa anapambana nacho ni kutengeneza mabadiliko na kufanya vizuri.


Achana na mashabiki, wachezaji ndiyo wako karibu zaidi na kocha wao na wanapaswa kumshikilia na kuhakikisha anafanya vema kwa maana ya kupotea maelekezo yake na kuongeza asilimia zao za ubora wa ufanisi ili kufikisha kile ambacho anakuwa amewapa.

 

Kwa wachezaji bado wanapaswa kujituma na kuunganisha nguvu naye kwa kuwa kama wao watashindwa, basi hata yeye kama kocha atakuwa hana maana.


Benchi la ufundi ambalo litakuwa pamoja na kocha huyo, lina zaidi ya watu wanne ambao nao watahitajika kumpa ushirikiano, kuwa karibu naye na kumshauri sahihi kwa kuwa yeye ni mgeni.


Taratibu mengi kuhusiana na kikosi hicho atakwenda anajifunza na kuchanganya na yale ambayo atakuwa anashauriana na anaowangoza katika benchi la ufundi.


Baada ya wachezaji, mashabiki na benchi la ufundi. Uongozi nao bado utatakiwa kuwa na ushirikiano naye wa karibu kwa kutimiza yale yanayohitajika ili kuifanya kazi yake iwe na wepesi. Kama yameanza kufanyika, mwendelezo unahitajika.


Kikubwa nilitaka kuwakumbusha kwamba kuna mambo mengi ya kumfanya au kuuonyesha ule ubora wa Kaze. Maana hawezi kutimiza kila kitu mwenyewe na hata akiwa ana mazuri, kuna sehemu muda unahitajika, maana yake kwenu, uvumlivu lazima.