Home Uncategorized WAHOLANZI WAPEWA JUKUMU LA KUMLETA KOCHA MPYA WA YANGA BONGO

WAHOLANZI WAPEWA JUKUMU LA KUMLETA KOCHA MPYA WA YANGA BONGO

 


IMEBAINIKA kuwa wakati Mrundi Cedric Kaze, akijiandaa kuja kuchukua mikoba ya kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Waholanzi ndiyo ambao watahusika kumleta kocha huyo hapa nchini.

 

Waholanzi hao kupitia Shirika la Ndege la taifa hilo, KLM Royal Dutch Airlines (KLM), ndiyo watakaombeba Kaze kwa kumtoa Canada alipo kwa sasa na kumshusha katika ardhi ya Tanzania Alhamisi saa 4 usiku, maalum kuanza kazi kwenye kikosi hicho.

 

Kaze anatua Bongo kwa ajili ya kuungana na Yanga baada ya timu hiyo kusitisha mkataba wa Mserbia, Zlatko Krmpotić ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo.

 

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema ndege hiyo ya KLM ndiyo ambayo itahusika kumshusha kocha huyo hapa nchini. “Kocha atafika na ndege ya KLM, siku ya Alhamisi saa 4 usiku kwa ajili ya kuanza kazi,” alisema kwa kifupi Hersi.


Kwa sasa Yanga ipo mikononi mwa Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi inajiandaa na mechi zake za Ligi Kuu Bara ambapo mchezo wake unaofuata kwenye ligi ni dhidi ya Polisi Tanzania.


Mchezo huo utachezwa Oktoba 22, Uwanja wa Mkapa utakuwa ni wa sita kwa Yanga iliyo nafasi ya tatu na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano.

SOMA NA HII  KANE MAJANGA TUPU, HATIHATI KUUKOSA MCHEZO WA KUFUZU KOMBE LA DUNIA