PATRICK Aussems, Kocha wa zamani wa Simba maarufu kama uchebe imeripotiwa kuwa amefutwa kazi ndani ya timu yake mpya ya Black Leopard ambayo alikuwa akiifundisha ndani ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Aussems aliibukia ndani ya klabu hiyo baada ya mabosi wa timu hiyo kuvutiwa na uwezo wake wakati akiifundisha timu ya Simba ambayo nayo ilimfuta kazi kwa kile ilichoeleza kuwa kushindwa kufikia malengo ambayo waliyaweka kimataifa kwa kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akiwa ndani ya Smba aliweza kushinda taji la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2018/19 na aliifikisha timu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aussems raia wa Ubelgiji alipata dili la kuinoa Black Leopards msimu huu akiwa hana timu baada ya kuachana na Simba ambayo ipo chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck.
Kwa sasa inatajwa kuwa mikoba yake inaweza kuchukuliwa na kocha wa zamani wa Klabu ya Baroka FC Dylan Kerr.
Sababu ya kupigwa chini ndani ya timu hiyo inaelezwa kuwa ni matokeo mabovu ya timu hiyo kwa kuwa kwenye mechi tatu za mwanzo ameshindwa kupata ushindi.