KAMPUNI ya Azam Media imefanya maboresho makubwa kwa wateja wake wote nchini na nchi jirani sambamba na kutambulisha Visimbuzi vya Kidigitali.
Uzinduzi huo ulifanyika usiku wa kuamkia leo Hyatt Regency Dar es Salaam The Kilimanjaro jijini Dar.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji (C.E.O) wa Azam Televisheni Limited, Sabrina Mohamedali amesema kuwa maboresho hayo wameyafanya kwa ajili ya kuwaridhisha zaidi wateja nchini na nje ya nchi.
Sabrina amesema kuwa maboresho hayo ni katika kuzingatia kuongeza ubora na kujidhatiti katika kuwaletea wateja wao bidhaa za kisasa ambazo zitakidhi mahitaji yao kwa bei nafuu zaidi.
Aliongeza kuwa maboresho mengine ya kuleta Visimbuzi vya Kidigitali vinavyotumia mfumo wa antena.
“Lengo letu kubwa la kuja na teknolojia hii ya kisasa kabisa ni kutimiza malengo yetu ya kuwafikia wengi zaidi nchini.
” Uzuri wa Visimbuzi hivi ni kuwa haviathiri na mabadiliko ya hali ya hewa na pia unaweza ukajiunganishia wewe mwenyewe kwa uwepesi na haraka zaidi.
“Kisimbusi hichi kitapatikana sokoni kwa wateja wetu kwa bei nafuu sana ya Shilingi 99, 000 tu kuanzia Desemba Mosi, mwaka huu na mauzo yataanzia jijini Dar es Salaam na kisha kuendelea kwenye mikoa mingine.
” Kingine tumeboresha makubwa tuliyoyafanya ni kuongeza chaneli na vipindi zaidi vyenye mvuto kwa kila mtu na kila rika na kila jinsia,” amesema Sabrina na kuongeza kuwa “Tumeingia katika ushirikiano na Wasafi TV ambapo kuanzia Desemba Mosi, mwaka huu wateja wetu wa vifurushi vyote wataipata chaneli ya Wasafi TV bila ya malipo ya ziada.
Aidha, Sabrina alitangaza kutangaza mapunguzo ya bei ya vifurushi ambavyo vitakuwa hivi; Vifurushi cha Lite kitapatika kwa Shilingi 8000, Kifurushi cha Pure Shilingi 13, 000 na Kifurushi cha Plus Shilingi 20, 000.