KOCHA Mkuu wa Liverpool amesema kuwa kucheza mbele ya mashabiki 2,000 Uwanja wa Anfield ni sababu ya wachezaji wake kufanya maajabu na kushinda mabao 4-0 dhidi ya Wolves huku mikono ya kipa Caoimhin Kelleher ikiweka lango la Jurgen Klopp salama.
Klopp amesema kuwa kukaa miezi 10 bila ya mashabiki ndani ya uwanja kulikuwa kukiwapa presha wachezaji wake hasa ukizingatia kwamba safu yake ya ulinzi wengi wanasumbuliwa na majeraha hivyo uwepo wa mashabiki uliwapa nguvu ya kupambana zaidi.
Mashabiki walikuwa wamezuiwa kuingia ndani ya uwanja kutokana na mapambano dhidi ya Virusi vya Corona ambavyo bado vinaisumbua dunia, hata wale 2,000 walioingia walipaswa kuchukua tahadhari ili kujilinda zaidi.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Mohamed Salah dakika ya 24, Georginio Wijnaldum dk ya 58, Joe Matip dk 67 na Nelsone Semedo alijifunga dk ya 78 na kuwafanya mabingwa hao watetezi kufikisha jumla ya pointi 24 wakiwa nafasi ya pili na vinara ni Tottenham ambao wametofautiana kwenye idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Klopp amesema:” Baada ya miezi 10 kupita bila ya uwepo wa mashabiki ninadhani kutokea kwao ndani ya uwanja kwetu imetupa nguvu na tumeweza kufanya maajabu hasa kwa uwepo wa mashabiki ndani ya uwanja.
“Sawa, tumewapata mashabiki baada ya muda kupita lakini inabidi wajue kwamba tupo tayari katika kufanya mambo mazuri, huu ni mwanzo tu, wametufanya tujihisi vizuri hasa pale ambapo wanaimba,” amesema.