GOLBE Elisha, mwili jumba nyota wa kikosi cha Plateau United ambaye ni nahodha wa kikosi hicho kilichoondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa hatua ya awali na Simba, amesema kuwa kikwazo namba moja ilikuwa ni Luis Miquissone.
Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa New Jos, nchini Nigeria Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Clatous Chama jambo lililowapa faida Simba kutinga hatua ya mtoano baada ya suluhu ya juzi Uwanja wa Mkapa.
Elisha amesema kuwa walishindwa kupata matokeo mchezo wa kwanza nyumbani kutokana na uwepo wa Luis jambo lililowavuruga jumlajumla.
“Mchezo wetu wa kwanza nyumbani tulivurugwa kabisa na wachezaji wengi wa Simba ila waliongozwa na kiana mfupi jezi yake ni namba 11,(Luis) na aliyefunga bao kwenye mchezo huo,(Clatous Chama).
“Yule kijana (Luis) ni alituvuruga mwanzo mwisho kwa kuwa alikuwa akivuruga mipango yetu na mpaka sasa tukashindwa kupata ushindi, ila yote kwa yote wanastahili pongezi,” amesema.
Luis kwenye mchezo wa marudio Desemba 5, Uwanja wa Mkapa aliwavuruga Plateau United kwa kucheza anavyotaka jambo ambalo lilimsababishia awekwe chini ya Ali Issa ambaye alipewa jukumu la kumkaba.
Licha ya kuwekwa chini ya ulinzi huo dakika ya 64 alisepa na kijiji chake kwa kuwapiga chenga za maudhi nyota watano na kutoa pasi ya uhakika kwa Chama ambayo ilileta kona.