IMEELEZWA kuwa mpango wa nyota wa zamani wa kikosi cha Simba Emmanuel Okwi kurejea ndani ya Simba kwa sasa umefikia sehemu nzuri baada ya jina lake kuwa mezani kwa mabosi wakilijadili upya ili kuweza kumrejesha kundini.
Nyota huyo raia wa Uganda amekuwa akihusishwa kurejea tena Bongo ili kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuiaji ya Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Okwi ana uzoefu na ligi ya Tanzania akiwa amecheza timu zote za Kariakoo ambazo ni Simba na Yanga anaweza kuibuka muda wowote kuanzia sasa ikiwa Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck atakubali atue.
Habari kutoka chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa Okwi yeye mwenyewe ameomba kurejea kikosini hapo baada ya kukumbuka pacha yake na Clatous Chama pamoja na Meddie Kagere namna ilivyofanya vizuri msimu wa 2018/19.
“Okwi ameomba kurudi Simba hasa baada ya kukukmbuka ile pacha yake aliyokuwa ameitengeneza Simba dhidi yake yeye, Kagere, John Bocco na Chama.
“Kilichobaki kwa sasa ni kuona namna gani hilo dili lake linaweza kupita kwani mabosi wanajadili ili kuona ikiwa anaweza kuwafaa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ama atafutwe mbadala wake.
“Ikiwa Sven atakubali aletwe basi ni suala la muda tu kwani Simba inahitaji kupata mshambuliaji mmoja ambaye atakuwa msaidizi wa Bocco na Kagere pale mambo yanapokuwa magumu ndani ya kikosi,” ilieleza taarifa hiyo.
Meneja wa timu ya Simba, Abbas Ally amesema kuwa suala la Okwi bado halijawa rasmi mezani.
“Kuhusu Okwi (Emmanuel) hata sisi pia Simba tunaliskia kwenye vyombo vya habari kama ambavyo nyie mnaliskia ila bado halijawa rasmi,” amesema.
Kwa sasa Okwi anakipiga ndani ya Klabu ya Ittihad ya nchini Misri akiwa amecheza jumla ya mechi 14 na kutupia mabao mawili.
Chanzo:Championi