Home Uncategorized SIMBA NI CHAMA NA BOCCO TU..!!

SIMBA NI CHAMA NA BOCCO TU..!!

 Kasi ambayo Yanga inaenda nayo kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ni kama inawavuruga mabingwa watetezi wa ligi hiyo Simba, ambao juzi walipata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Licha ya Mbeya City kuwa ya tatu kutoka chini ya misamo wa ligi, iliibana Simba katika mchezo huo na kama ingeongeza kasi kidogo mchezo ungemalizika kwa sare.

Simba inacheza mechi zake katika presha ya kutetea ubingwa wao na kusaka taji la nne mfululizo la ubingwa msimu huu, huku kasi ya wapinzani wao wakubwa, Yanga ambayo imeanza kufunga idadi kubwa ya mabao katika mechi zake ikizidi kuwachanganya.

Miamba hiyo imezidiwa na Yanga pointi nane, huku pia ikiwa na mechi mbili mkononi za viporo dhidi ya KMC wanayocheza nayo Jumatano na dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.

Ukiondoa mechi hizo, Simba ina mechi nne, mbili za kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi dhidi ya Namungo iliyopangwa kufanyika Jumapili na dhidi ya Azam itakayofanyika Desemba 27, wakati watani zao, Yanga wakiwa na michezo miwili dhidi ya Dodoma Jiji (Desemba 19) na itamaliza mzunguko wa kwanza kwa kucheza na Ihefu ugenini Desemba 26.

Kocha Sven bado haeleweki kwani katika mechi mbili zilizopita amekipangua kikosi chake hivyo watu kuhoji ni presha ya kutafuta matokeo akiikimbiza Yanga iliyo kileleni au anawapumzisha kutokana na pia kukabiliwa na mashindano ya kimataifa.

Katika mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania, aliwaweka benchi, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, John Bocco na Clatous Chama huku akiwaanzisha kikosi cha kwanza Gadiel Michael, Ibrahim Ame, Benard Morrison na Francis Kahata.

Hata hivyo, mambo yalipokua magumu zaidi eneo la ushambuliaji dakika ya 62 aliwatoa Kahata na Morrison na kuwaingiza Chama na Bocco na dakika mbili baadaye, Chama aliipatia Simba bao la kwanza akimalizia pasi ya Bocco, huku pia akifunga la pili dakika ya 90 na kuipa Simba pointi tatu muhimu.

Sven alipangua tena kikosi katika mchezo wa juzi dhidi ya Mbeya City kwa kuwapumzisha beki Pascal Wawa na winga Luis Miquisone nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Ame na Hassan Dilunga.

SOMA NA HII  AZAM MEDIA YABORESHA HUDUMA,YAZINDUA KISIMBUSI CHA DIGITAL

Ni wachezaji wale wale wa awali wakimpa tena Sven pointi tatu ugenini, kwani pasi ya Chama ilitendewa haki na Bocco katika ushindi wa bao 1-0, hivyo kuwafanya wawili hao kuwa roho ya kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Akizungumzia hali hiyo, kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Dar United, Mrage Kabange alisema Simba haitakiwi kucheza kwa kuiangalia Yanga kama inataka kushinda mechi zake na kutetea ubingwa msimu huu.

“Hapa hakuna namna kila mtu ashinde mechi zake mwisho wa msimu atajulikana nani mbabe wa mwenzake, lakini kama wanataka kuharibu basi waingie katika mkumbo wa presha dhidi ya Yanga, wanaweza kupoteza kabisa. Bado wana nafasi ya kurejea kileleni na hata kutwaa ubingwa kama wakitulia na kucheza kwenye ubora wao,” alisema Mrage.

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Ally Mayay alisema Simba na Yanga miaka yote lazima mmoja akifanya vizuri, mwingine atakuwa katika presha kubwa.

“Simba kwa sasa kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wako vizuri, lakini kipindi cha pili huwa nguvu yao inapungua, sijui kwanini, labda ni wachezaji wanachoka au ni mikakati ya kocha wao, lakini wanatakiwa kucheza bila kuiangalia Yanga inafanya nini,” alisema Mayay.