MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, ameahidi kufunga usajili wa dirisha dogo na straika mmoja bora ukanda wa Afrika zaidi ya Mrundi, Said Ntibazonkiza ‘Saido’.
Washambuliaji wanaotajwa kuwaniwa na Yanga ni Justin Shonga anayekipiga Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Mkongomani Dark Kabangu anayeichezea Klabu ya Motema Pembe ya nchini DR Congo.
Yanga tayari imekamilisha usajili wa mchezaji mmoja pekee katika usajili huu wa dirisha dogo lililofunguliwa Desemba 16, mwaka huu ambaye ni Saido aliyeanza kuitumikia timu hiyo akicheza michezo miwili ya Ligi Kuu Bara akifunga bao moja na kupiga asisti tatu.
Hersi amesema kuwa katika kutengeneza na kurejesha heshima ya timu hiyo, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Kocha Mkuu Mrundi Cedric Kaze wamepanga kukiboresha kikosi kwa kusajili mshambuliaji huyo mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao.
Hersi amesema kuwa wapo katika taratibu za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji huyo na klabu yake anayoichezea kutua nchini kwa ajili ya kukamilisha usajili wake utakaotikisa Afrika.
Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo atakayekuja ataingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, lengo likiwa ni kutwaa taji la ubingwa katika msimu huu waliomaliza mzunguko wa kwanza bila ya kufungwa.
“Baada ya kumaliza mzunguko huu wa kwanza wa ligi bila ya kufungwa, tumepanga usajili mmoja mkubwa wa mshambuliaji ndani ya Yanga katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo ambalo lipo wazi hivi sasa.
“Nikuhakikishie kuwa tupo katika mazungumzo ya mwisho na mshambuliaji huyo tishio ukanda wa Afrika ambaye jina lake ni siri hivi sasa na tumepanga kumtangaza mara baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili.
“Hivyo, niwahakikishie Wanayanga kuwa dirisha hili dogo la usajili ni lazima tumlete mshambiliaji bora atakayeingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kwa Saido ambaye hivi sasa ni tegemeo katika timu licha ya kucheza michezo miwili ya ligi,” amesema Hersi.