Home Uncategorized MGOMBEA SIMBA APEWA MILIONI

MGOMBEA SIMBA APEWA MILIONI


 ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali, amesema kuwa, wanachama zaidi ya 50 wamemfuata kumtaka kuwania nafasi ya uenyekiti ndani ya klabu hiyo ambapo tayari ameshafanikiwa kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

 

Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba, imetangaza uchaguzi mdogo ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya kuziba nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti, Swedi Mkwabi aliyeachia madaraka Septemba, mwaka jana ambapo nafasi hiyo ilikaimiwa na mjumbe wa kamati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mwina Kaduguda.

 

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Februari 7 mwakani ambapo zoezi la uchukuaji fomu limeanza Desemba 14 na litafungwa Desemba 24 huku wajumbe watatu wakijitokeza kuchukua fomu hizo.

 

 Dalali amesema kuwa, ameamua kuchukua fomu hiyo kutokana na kukidhi vigezo na ni haki yake kisheria kutokana na kanuni ya TFF ambayo inaruhusu mgombea mwenye elimu ya kidato cha nne.

 

“Nimechukua fomu kutokana na wanachama kunifuata nyumbani kwangu kuhitaji nifanye hivyo ambao wamenichangia fedha ya kwenda kuchukulia fomu kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000).

 

“Haina shida iwapo mimi nilikuwa mwenyekiti awali kwa kuwa sikuongoza miaka nane mfululizo, kikanuni inaeleza kuwa iwapo umekuwa mwenyekiti kwa muda wa miaka minne kisha ukaishia hapo na ukakaa pembeni na ukihitaji kugombea tena unaruhusiwa.


 “Nisingeweza kuruhusiwa kugombea iwapo ningekuwa nimeongoza kwa miaka nane mfululizo, kipindi kile sikuweza kugombea kutokana na vigezo vilivyowekwa vya elimu ya digrii lakini sasa uchaguzi unakwenda kwa mujibu wa kanuni ya TFF ambayo inaruhusu mtu kugombea akiwa na elimu ya kidato cha nne,” amesema Dalali.

 

Aidha miongoni mwa wanachama waliojitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Mohamed Soloka, Ayubu Semvua na Dalali.


Chanzo:Championi

SOMA NA HII  LEWANDOWSKI ANAKIMBIZIA REKODI TU