Home Uncategorized YACOUBA WA YANGA AWAPOTEZA CHAMA NA LUIS MAZIMA

YACOUBA WA YANGA AWAPOTEZA CHAMA NA LUIS MAZIMA


 YACOUBA Songne nyota wa Klabu ya Yanga ameweka rekodi yake ndani ya msimu wa 2020/21 kwa kuwapoteza nyota wawili tegemeo ndani ya Simba, Clatous Chama na Luis Miquissone, katika kuhusika na mabao mengi ndani ya mchezo mmoja.

 

Nyota huyo amezifuta rekodi za Chama na Luis ambazo waliziweka Uwanja wa Mkapa wakati wakiwa na timu zao ambapo walihusika kwenye mabao matatu huku yeye akihusika kwenye mabao manne ndani ya dakika 90.


Chama na Luis ambao wanacheza ndani ya Simba walianza kuweka rekodi hiyo kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Mkapa. Wakati Simba ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Biashara United, Chama alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja na kumfanya ahusike kwenye mabao matatu.

 

Luis yeye anashikilia rekodi ya kutoa ‘hat trick’ ya asisti ambapo alitoa jumla ya pasi tatu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 20.

 

Songne mwenye rasta za kubana kichwani alifuta rekodi hizo, Desemba 12 ambapo aliandika rekodi ya kibabe akiwa nje ya Dar, Uwanja wa Kambarage kwa kufunga mabao mawili na kutoa asisti mbili na kumfanya ahusike kwenye jumla ya mabao manne wakati Yanga ikishinda mabao 5-0 dhidi ya Mwadui FC.


Ushindi huo unaifanya Yanga iweze kuweka rekodi kwa msimu wa 2020/21, kupata ushindi mkubwa ndani ya uwanja kwa kuwa mchezo wa mwisho kushinda mabao mengi msimu huu ilikuwa ni wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union.

 

Yanga ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 15, ikiwaacha Simba kwa jumla ya pointi 8 ambao wamecheza mechi 13 na pointi zao 29.

SOMA NA HII  BURUNDI WATIA TIMU BONGO, TAYARI KUIVAA STARS