Home Ligi Kuu HIKI HAPA KIKOSI CHA USAJILI BORA LIGI KUU BARA

HIKI HAPA KIKOSI CHA USAJILI BORA LIGI KUU BARA


LENGO kubwa la usajili wowote ule ni kuboresha pale ambapo palionekana kuna mapengo kwenye timu fulani kwa kuongeza mchezaji.

Siku 30 za usajili wa dirisha dogo la usajili Bara zilifungwa wiki iliyopita huku ikishuhudia timu karibu zote zikiwa na maingizo ya wachezaji wapya vikosini mwao. Lakini katika usajili huo kuna sajili ambazo zinaonekana kuwa bora zaidi kama ifuatavyo;

Kipa: Mathias Kigonya – Azam

Licha ya kuwa na orodha pana kidogo ya makipa ambao wamesajiliwa kwenye dirisha hili lakini Mganda Mathias Kigonya ndio unaonekana kuwa bora zaidi.

Kipa aliyetua Azam FC akitokea Forest Rangers ya Zambia licha ya kudaka lakini pia anafunga, akiwa amekuja kwa ajili ya kuwasaidia David Kissu na Benedict Haule.

Makipa wengine waliosajiliwa dirisha hili ni Deogratius Munishi (Ihefu), Ally Mustapha (Mbeya City) na Peter Manyika (Dodoma Jiji).

Mabeki wa pembeni; Edward Manyama na Ally Ally

Usajili wa Edward Charles Manyama kutoka Namungo kwenda Ruvu Shooting umewashtua wengi, kwani haukutarajiwa kutokea lakini haumuondoi beki huyo kuwa kwenye kikosi hiki anaingia kama mlinzi wa kushoto.

Lakini pia Ally Ally ambaye ametua Coastal Union akitokea kwao Zanzibar unamfanya awe miongoni mwa wachezaji ambao wakiunda kikosi cha usajili bora basi atakuwepo akiwa kama mlinzi wa kulia.

Mabeki wa kati; Job na Kelvin Yondani

Hapa hakuna shaka yoyote kwamba mabeki hawa wanastahili kuanza katika kikosi hiki wakiwa kama walinzi wa kati. Yondani amerejea kwenye ligi akisaini Polisi Tanzania baada ya kutokuwa na timu kwa miezi sita.

Job ametua Yanga akitokea Mtibwa Sugar ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu. 

Kiungo mkabaji; Taddeo Lwanga

Kiungo huyu raia wa Uganda kasi yake inaonekana kuongezeka kila baada ya mechi tofauti na mwanzoni wakati anaanza kucheza.

Lwanga amesaini Simba na kumwaga winbo kwake ndani ya Msimbazi kunamuweka katika kikosi cha usajili bora ambao umefanywa kipindi cha dirisha dogo.

Kiungo mchezeshaji; Raphael Daud

Kiungo huyu amerejea tena uwanjani akiwa na Ihefu SC baada ya kutokuwa na timu tangu kuanza kwa msimu huu. Licha ya kwamba hajacheza lakini kama pakiundwa kikosi cha usajili bora basi Raphael hawezi kukosa nafasi kwenye eneo la kiungo mshambuliaji.

SOMA NA HII  FT: YANGA 1-0 MTIBWA SUGAR

Mawinga; Perfect Chikwende na Erick Kwizera

Hawa wote ni wageni, mmoja akitokea Zimbabwe na mwingine Burundi. Wote wameonyesha pafomansi nzuri ambapo mabosi wa Simba walipagawa Chikwende akiwa FC Platinum ambapo aliwafunga na mwisho wakamsajili.

Kwizera raia wa Burundi alithibitisha uwezo wake kwenye Kombe la Mapinduzi akiwa na jezi za Namungo kiasi mabosi wa klabu hiyo wakampa mkataba. Katika kikosi hiki wawili hawa ndio watakuwa mawinga.

Washambuliaji; Reliants Lusajo na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’

Mabwana hawa ndio ambao watasimama eneo la ushambuliaji na tayari kila mmoja kazi yao wameshaionesha. Lusajo akiwa na KMC kabla ya kutua Namungo alifunga mabao manne.

Saido ameshafunga mabao mawili na ana pasi tatu za mabao hadi sasa ikiwa ni baada ya kusajiliwa Yanga akiwa mchezaji huru.

Wachezaji wa akiba

Deogratius Munishi ‘Dida’ (Ihefu), Yusuf Mlipili (Kagera Sugar), Yahya Zayd (Azam), Fiston Abdoul Razak (Yanga), David Mwasa (Mbeya City) na Mrisho Ngassa (Gwambina).