Home Uncategorized SIMBA INA KAZI KUBWA YA KUFANYA LEO MBELE YA WAZIMBABWE, REKODI HAZICHEZI

SIMBA INA KAZI KUBWA YA KUFANYA LEO MBELE YA WAZIMBABWE, REKODI HAZICHEZI

 


SIMBA wanatarajiwa kuwa uwanjani jioni ya leo Jumatano kucheza dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe katika mchezo wa pili wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Huo ni mchezo wa lazima kwa Simba kushinda tena kwa tofauti ya mabao mawili na kuendelea, kufanya hivyo inamaanisha kuwa kutawawezesha wao kusonga mbele na kuingia katika Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Kama Simba watafuzu litakuwa jambo zuri na kama Mtanzania natamani wapige hatua mbele zaidi kwa kuwa ni wawakilishi wa taifa na pili, mafanikio yao ni kuongezeka kwa pointi za ubora wa klabu kwa Tanzania, kitu ambacho kinaweza kusababisha tuongeze washiriki wengi katika michuano ya kimataifa msimu ujao.

 

Hilo linajulikana kwani msimu kadhaa nyuma wakati timu zetu ngazi ya klabu zilipofanikiwa kufanya vizuri kiasi, zilichangia kuongezeka kwa wawakilishi kutoka Tanzania ngazi ya kimataifa.


Lakini kabla sijauzungumzia mchezo wa leo, nikukumbushe kitu kuhusu safari kama hii ambayo Simba wanaenda kuindeleza leo pale Uwanja wa Mkapa.


Msimu wa 2018/19, ikicheza kwenye uwanja huohuo wa Mkapa, Simba ililazimika kufanya kazi ya ziada na kupata ushindi wa mabao 3-1 dakika za mwisho dhidi ya Nkana ya Zambia.Mchezo wa awali Simba ilifungwa mabao 2-1 ugenini, iliporejea nchini dakika za mwanzo tu Simba wakafungwa bao moja huku umati wa mashabiki ukiwa ni wa kiwango cha juu.

 

Ilionekana kama safari ya Simba imefikia mwisho kwa kuwa hapo matokeo yalisomeka 3-1, hamasa, ubora na uenyeji ukafanya Simba waongeze bidii na mwisho Chama akafunga bao la kisigino ambalo ilikuwa ni zaidi ya shangwe kwa wanokumbuka siku hiyo.


Simba ilisonga mbele na kuingia hatua ya makundi ambapo huko nako ilifanya vizuri.

 

Msimu uliopita wakati matumaini yakiwa ni makubwa kutokana na kile kilichotokea msimu uliomalizika. Wanasimba wengi wakawa wanaiwaza nusu fainali ya ligi ya Mabingwa na kuondoa umakini wao katika hatua za awali ambazo walitakiwa kupita.

SOMA NA HII  HUKO AZAM SIO POA UNAAMBIWA MASTAA HAWAMTAKI KOCHA.......HUKU MABOSI NAO WAZIBA MASIKIO

 

Nahisi walijiona wameshakuwa wakubwa na wakajisahau kuwekeza nguvu katika hatua za awali wakiwa na imani kuwa huko watapita kirahisi.Msimu uliopita wa 2019/20, Simba baada ya kutoka suluhu ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji, wakaamini kama waliweza kuwafunga vigogo wengi ndani ya Uwanja wa Mkapa, hao UD Songo hawakuwa na nguvu ya kuwazuia wao kufanya kile walichokifanya.


Bao la Luis Misquissone katika dakika ya 14 likatibua sherehe ya Wanasimba wote, licha ya kupambana kwa nguvu waliishia kupata sare ya bao 1-1, Erasto Nyoni akifunga kwa penalti dakika ya 85.


Ilikuwa ni kama anguko kubwa kwa Simba, hawakutegemea kilichotokea, hata Watanzania wengi ni kama waliona maajabu kwa kilichotokea, lakini huo ndiyo ukweli.

 

Msimu huu kwa mara nyingine Simba wanashiriki michuano hiyo, kuanzia hatua ya awali walipangwa na timu ngumu na zimewatoa jasho hasa.Baada ya kuwatoa Plateau United ya Nigeria, sasa wana kazi nzito ya kumaliza kazi na FC Platinum.

 

Kumekuwa na imani kubwa kwa Wanasimba kuwa rekodi yao ya kwa Mkapa ni zuri, sawa lakini hiyo haimaanishi kuwa watapita kirahisi.

 

Mchezo huu hawatakiwi kuuchukulia kuwa lazima watashinda kwa kuwa tu wana rekodi nzuri nyumbani, kazi inatakiwa kufanyika, imani kama hiyo ilikuwa msimu uliopita dhidi ya UD Songo, kutokea tena safari hii kunaweza kuwa pigo zito.

 

Wakati hizi propaganda za mashabiki na wadau wa Simba nje ya uwanja zikiendelea, viongozi wa Simba na benchi lao la ufundi wanatakiwa kuelekeza nguvu na mbinu za kuanzia nje hadi ndani ya uwanja kuhakikisha matokeo yanapatikana na siyo wao kuishi kwa historia kama mashabiki wanavyofikiria.