KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes Da Rosa, amefunguka kuwa kama watacheza kwa nidhamu na kupambana pamoja kama walivyofanya kwenye mchezo uliopita dhidi ya AS Vita, basi ni wazi watafika mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Simba ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Ijumaa iliyopita ilianza vizuri michezo ya hatua ya makundi kwa kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya AS Vita.
Ushindi huo umeifanya Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Kundi A la michunao hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika lililo na timu za Al Ahly, Simba, Al Merrikh na AS Vita.
Leo Al Ahly itacheza dhidi ya Al Merrikh.Mchezo ujao kwa Simba ni ule watakaocheza nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly utakaopigwa Februari 23, mwaka huu katika Dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Spoti Xtra, kuhusu nafasi ya Simba kwenye michuano hiyo, Gomes alisema: “Naiona nafasi ya kikosi changu kufika mbali zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kama tu tutaweza kucheza kwa nidhamu na kupambana pamoja kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita dhidi ya AS Vita.
“Tulicheza vizuri sana, licha ya kwamba hatukutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini niseme kuwa niliri-dhishwa na kiwango cha nidhamu na roho ya upambanaji kwa vijana wangu.