MATOKEO ya Simba 2-3 Mashujaa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Desemba 26,2018 yamewaogopesha Simba na kuwafanya waongeze umakini kuikabili leo African Lyon.
Zama za Patrick Aussems alipomuamini kipa namba mbili Deogratius Munish na mshambuliaji wake Adam Salamba walikutana na balaa hilo jambo ambalo leo uongozi haupendi kuona likitokea tena.
Majira ya saa 1:00 usiku, Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes itakuwa na kibarua cha kufanya mbele ya African Lyon ambao ni wenyeji kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 32 bora.
Simba ni mabingwa watetezi wanakutana na African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na hesabu za kuwavua ubingwa ili iweze kushiriki mashindano ya kimataifa.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa wanakumbuka kilichowakuta mbele ya Mashujaa Uwanja wa Mkapa hivyo wataingia kwa nidhamu mbele ya wapinzani wao.
“Tunatambua kwamba tumeshawahi kupoteza kwenye mechi zetu za Kombe la Shirikisho mbele ya Mashujaa pia iliwahi kutokea mbele ya Green Warriors hivyo tunawaheshimu wapinzani wetu na tutapambana ili kupata matokeo.
“Uzuri ni kwamba kila mchezaji anajua malengo ambayo tunayo na hesabu zetu ni kupata matokeo chanya. Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri ila tunawaheshimu wapinzani wetu,”.