BAADA ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba, Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane, ameibuka na kutamka kuwa Simba ilikuwa kwenye ubora zaidi ya wao.Kocha huyo alisema kati ya nyota ambao aliwaona ni hatari kwao ni mfungaji pekee wa bao hilo, Luis Miquissone na beki wa kati, Joash Onyango.
Akizungumza na Spoti Xtra, kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema katika mchezo huo wachezaji wake hawakuwa na kasi anayoifahamu tofauti na wapinzani wao Simba walioonekana kulishambulia goli lao dakika zote tisini.
Kocha huyo alisema Simba walitumia vema udhaifu wao na kufanikiwa kupata ushindi huo “Niwe muwazi tu kwa kusema hatukuwa na kasi uwanjani na Simba wakawa bora, hivyo wakatumia vema udhaifu wetu kutudhuru na kufanikiwa kupata pointi tatu dhidi yetu.
“Simba walifanikiwa kucheza kwa nguvu na kujilinda vizuri kwa dakika zote 90. Walikuwa makini katika kuokoa mipira yote ya hatari iliyokuwa inafika golini kwao. Wachezaji hatari alikuwa mwenye namba 11 (Luis) na 16 (Onyango),” alisema Mosimane.