Home Simba SC NAKUKUMBUSHA TU SUPER CUP YA SIMBA ILIVYOENDESHA MAISHA…

NAKUKUMBUSHA TU SUPER CUP YA SIMBA ILIVYOENDESHA MAISHA…

 

NA SALEH ALLY

KLABU ya Simba iliamua kubuni michuano yake maalum kama Simba Super Cup ambayo imefikia tamati jana kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kwa kila timu kucheza mechi mbili.

Vigogo wa Afrika TP Mazembe kutoka DR Congo na vigogo wengine Al Hilal ya Sudan walikaribishwa na wababe wa soka la Tanzania kwa kipindi hiki, Simba.

Ilikuwa michuano ya wababe, michuano ya klabu tatu kubwa za Afrika ambazo ziko katika michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika zikipambana kupata fedha na heshima pia.

Nguvu ya michuano hiyo imeonekana kwa maana ya burudani, kila timu imeonyesha uwezo na mambo yalikuwa mazuri wakati Al Hilal ilipoanza kwa kutandikwa kwa mabao 4-1 na wenyeji Simba, huenda watu walidhani wao ni vibonde lakini mechi ya pili, wakawatuliza Mazembe kwa mabao 2-1.

Hii ilifanya mashindano haya yawe na raha zaidi na hata mashabiki kujitokeza kwa wingi zaidi kuishuhudia michuano hiyo kwa maana ya mechi ya mwisho iliyowakutanisha Simba dhidi ya TP Mazembe, jana.

Michuano hiyo imeacha burudani kwa mashabiki ambao walikwenda uwanjani au kwa wale walioshuhudia kupitia Azam TV ambao walinunua haki za kuonyesha michuano hiyo.

Mashabiki wameona mengi ya kujifunza kutoka kwa Al Hilal na TP Mazembe ambao kuwaona wakija nchini na kucheza ilikuwa ni lazima wapangwe na timu ya hapa nyumbani na mara nyingi imekuwa ni Yanga au Simba kwa kuwa ndio wenye nafasi kubwa zaidi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Safari hii wamewaona, tena wakicheza mechi mbili, moja na wageni wenzao na nyingine na timu ya nyumbani. Mashabiki wa Simba wakaishangilia timu yao dhidi ya Mazembe na wale wa Yanga wakaburudika kwa kuizodoa, hii ni raha ya kimpira.

Pamoja na hivyo, tunakwenda kukubaliana kwamba michuano hiyo imekuwa na faida, Simba wametengeneza kitu ambacho kimekuwa kwa jamii na Serikali ya Tanzania na faida hizi hazijali hata kidogo ushabiki.

SOMA NA HII  SIMBA WAJA NA POINTI OF NO RETURN KUWAKABILI WAARABU

Unaona, ukianzia wale wa biashara ndogondogo kwa maana ya wachuuzi au wajasiriamali wamefanikiwa kuingiza fedha wakati wakifanya biashara zao pale Uwanja wa Mkapa, iwe ndani au nje.

Wako wameuza tiketi za mechi hiyo na kujiingizia kipato, magari yamewabeba na kuwapeleka au kuwarudisha waliokwenda kuangalia mechi na wengine wengi ambao wameingiza fedha kupitia mechi hiyo.

 

Achana na hivyo, kuna wale wa kwenye mahoteli ambao wachezaji wa timu hizo walifikia. Nao waliingiza kiasi kikubwa cha fedha hata kama kutakuwa na punguzo ambalo walilazimika kulifanya lakini katika kipindi hiki dunia inahangaika na Corona, wateja wamekuwa wa shida hata hapa Tanzania ambako mambo ni tofauti kidogo.

Hawa ni wafanyabiashara lakini bado kuna wadau ambao ukiachana na mashabiki, mfano makocha, watakuwa wamejifunza jambo kupitia makocha wa timu hizi kubwa, hali kadhalika wachezaji na hata waandishi wa habari.

Nimeanza na mifano mingine nikitaka kulainisha ujue nakwenda kuangukia wapi. Lengo lilikuwa ni kutaka kukumbusha kwamba walichokifanya Simba katika Simba Super Cup kitufikirishe, ni kitu kizuri na kinapaswa kuungwa mkono na ikiwezekana kuigwa.

Tusione haya kuiga, ni kitu kizuri na bora kabisa. Kitu ambacho kina mengi yenye faida na unaona kama Yanga kutokana na nguvu ya mashabiki wakiwanacho, itakuwaje? Lazima kutakuwa na faida zake ambazo zitaigusa jamii. 

Hivyo wenye nafasi ya kuanzisha au kuiangalia hii na kubuni kingine, wasione haya, wafanye kwa kuwa dunia inaanza na kujifunza halafu unafanya.