Home Yanga SC KATIBU YANGA:- KAMATI YA USAJILI YA YANGA NI ‘JIPU’

KATIBU YANGA:- KAMATI YA USAJILI YA YANGA NI ‘JIPU’

 


ALIYEKUWA katibu muenezi wa Yanga, Abdallah Sauko ameunga mkono maamuzi ya uongozi kumtimua kocha Cedrick Kaze, lakini ameamua kutumbua jipu katika kamati ya usajili iliyoleta wachezaji ambao hawana msaada.

Sauko ameiambia TOVUTI ya Mwanaspoti online, leo Jumatatu ya Machi 8, 2021 kwamba pamoja na Kaze kuzidiwa na ukubwa wa Yanga,  amehoji kamati ya usajili iliyoleta wachezaji wapya tangu mwaka juzi ihojiwe iliwatoa wapi na iliwasajili kwa vigezo gani.

Amewataja baadhi ya wachezaji waliosajiliwa kwa vipindi tofauti kama Juma Balinya, David Molinga, Micheal Sarpong, Fiston Abdulrazak  kwamba hakuna walichoisaidia timu zaidi ya kupiga pesa na kuondoka, jambo linalomfikirisha kwamba kwanini hawaguswi na kuambiwa ukweli.

“Mfano huyo Fiston hamzidi chochote  mchezaji mzawa Wazir Junior ambaye najiuliza kwanini  Kaze alikuwa anamuweka nje na anampa nafasi huyo Fistoni asiye na maajabu yoyote, yaani unaweza kuona shida ilivyo kwenye timu,” amesema na amengeza kuwa;

“Humo kwenye kamati ya usajili ya Yanga ndio kuna uozo, wapo watu ambao wana manufaa yao wenyewe, Yanga inasajili sana,mfano msimu uliopita na sasa hivi, kwanini wahusika wasiulizwe ili wajitafakari na jicho lao la kuona vipaji, bila kusema ukweli ni ngumu kuona kile tunachokitamani,” amesema.

Amesisitiza kwamba baada ya kuondoka Kaze, hiyo kamati inayosajili inatakiwa kutazamwa kwa jicho la kuleta mabadiliko yale mashabiki wanahitaji, lasivyo makosa na timuatimua itaendelea kama kawaida.

“Kama hautasemwa ukweli basi tutaendelea kushuhudia madudu, huu ni wakati ambao Yanga inatakiwa ifanye mapinduzi ya kweli ili kupata timu bora ambayo itakuwa inatamba ligi ya ndani na kimataifa,”amesema.

 

SOMA NA HII  GAMONDI AKOMAA NA MRITHI WA MAYELE, HAPO KAMBINI HAPAKALIKI