UWANJA wa Mkapa leo Machi 10 saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo mkali kati ya Simba inayonolewa na Didier Gomes na Prisons inayonolewa na Salum Mayanga.
Simba inakumbuka kwamba mchezo wa kwanza kuonja joto ya jiwe kwa kuyeyusha pointi tatu ilikuwa Uwanja wa Nelson Mandela ambapo ubao ulisoma Prisons 1-0 Simba.
Bao la Samson Mbangula lilitosha kuipa pointi tatu Tanzania Prisons na kuifanya Simba chini ya Sven Vandenbroeck kupoteza pointi zote tatu ugenini.
Hivyo leo Gomes ana kazi ya kulipa kisasi kwa ajili ya mechi iliyopita kwa kuwa watangulizi wake walikwama kusepa na pointi tatu mbele ya Wajelajela hao.
Salum Kimenya, kiraka wa Tanzania Prisons amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo ambao umeshika hisia za mashabiki wa timu hizo mbili.
“Sisi tumejiandaa vizuri na tunatambua kwamba tunakutana na wapinzani ambao nao wanahitaji pointi tatu kama ilivyo kwetu.
“Kikubwa ni kuona kwamba tunaweza kupata matokeo chanya jambo ambalo litazidi kutufanya tufikie malengo yetu ambayo tumejiwekea.” .
Kwa upande wa Simba, nahodha John Bocco amesema kuwa wachezaji wapo tayari kwa ajili ya ushindani uwanjani.
Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19 inakutana na Tanzania Prisons ambayo imecheza jumla ya mechi 21 na ina pointi 27.