Home Simba SC HIZI HAPA SABABU ZA MORRISON NA LOKOSA KUKOSEKANIKA KATIKA MSAFARA WA SUDANI

HIZI HAPA SABABU ZA MORRISON NA LOKOSA KUKOSEKANIKA KATIKA MSAFARA WA SUDANI


Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imeendelea kuwa mfupa mgumu kwa washambuliaji Bernard Morrison na Junior Lokosa baada ya nyota hao kuachwa katika kikosi cha wachezaji 25 wanaosafiri kwenda Sudan kuivaa Al Merreikh, Jumamosi hii.

Wakati nyota 27 wa Simba wakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa safari hiyo itakayoanza saa 10 jioni, Morrison na Lokosa hawamo kundi sambamba na nyota wengine watatu wa timu hiyo, Perfect Chikwende, Ibrahim Ame na Said Ndemla.

Hata hivyo, Chikwende ameachwa kwa sababu hatumiki katika mashindano hayo tofauti na wengine wanne walioachwa lakini sintofahamu kubwa iko kwa Morrison na Lokosa ambao hawajacheza hata mechi moja kati ya mbili ambazo Simba imeshacheza kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo dhidi ya AS Vita Club na Al Ahly.

Gumzo zaidi limekuwa kwa Lokosa aliyewahi kuichezea Esperence ya Tunisia ambaye Simba ilimsajili kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kwani hajawahi kukaa benchi hatak katika mchezo mmoja ingawa Mshauri wa Masuala ya Ufundi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba,  Crescentius Magori alisema hilo linatokana na uamuzi wa kocha.

“Hiyo ni maamuzi ya mwalimu kwa sababu mwalimu ana wachezaji 33 kwa hiyo kaangalia nafasi ya kucheza. Mwalimu ameangalia utayari wa wachezaji kwa sababu John Bocco amerudi labda ndio amechukua nafasi yake lakini siwezi kumuongelea mwalimu,” alisema Magori

Kwa upande wake, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kuwa wachezaji wote waliosafiri wana ari na morali kwa ajili ya mechi hiyo.

“Al Merreikh ni timu ambayo imekuwa na mabadiliko makubwa na imekuwa ikipata matokeo mazuri nje zaidi ya mara moja lakini tuko katika ngazi nzuri na mimi kurejea kwangu vilevile kunatakiwa kuonyesha kwamba natakiwa kuiondoa pale ilipofika kuipeleka mbele zaidi kwa kushirikiana na wenzangu.

Sasa tuna safari kwa hiyo la msingi akili, mawazo, nuvu na kila kitu tunatakiwa tukielekeze katika mechi hiyo. Ni mechi muhimu ukichukulia kwamba tunatakiwa tuhakikishe tunafika katika robo fainali na mbele ya safari tuangalie kama tunaweza kufika fainali.

SOMA NA HII  AHMED ALLY:- YANGA INAWACHEZAJI BORA SANA...

Tunakwenda na wachezaji 25 ambao wote wako katika hali nzuri kimwili, kiafya na kiakili na wote wana mwamko na hamu ya kwenda kupata matokeo. Kwa hiyo tumuombe Mungu tufike salama kwanza. Tukishafika tuna siku mbili tatu kuelekea mchezo husika tuamke salama.

Namini yale waliyoyafanya katika mchezo uliopita, watayafanya katika mchezo huu unaokuja.Msafara utakuwa na watu 40na kuna viongozi wengine wanakuja kesho na kuna waliotangulia jana kwa hiyo kiujumla unaweza kuwa na takribani watu 55,” alisema Rweyemamu