Home Simba SC MANULA AFUNGUKA HAYA KUHUSU TUKIO ZIMA LA KUZIMIA UWANJANI

MANULA AFUNGUKA HAYA KUHUSU TUKIO ZIMA LA KUZIMIA UWANJANI


Wakati msafara wa Simba ukiondoka jioni ya leo Machi 3 kuelekea Sudan kuwavaa Al Merreikh keshokutwa Jumamosi, kipa Aishi Manula ni miongoni mwa wachezaji waliomo katika kundi la nyota 27 watakaondoka leo kwenda katika mechi hiyo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kipa huyo alizua wasiwasi kuwa huenda asisafiri na timu baada ya kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, juzi Jumatatu ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Hata hivyo, baada ya matibabu aliyoyapata, kipa huyo amekuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba watakaoondoka jioni ya leo kwenda Sudan tayari kwa mchezo huo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa jijini Khartoum, keshokutwa Jumamosi.

Manula alisema kuwa kwa sasa afya yake inazidi kutengemaa na ana nafasi kubwa ya kucheza mechi ya keshokutwa ikiwa benchi la ufundi litampa nafasi.

“Kwanza namshukuru Mungu naendelea vizuri na hali yangu inazidi kuimarika kama walivyoona. Nilipata ajali katika hali ya mchezo ambayo ilipelekea kupoteza fahamu na mbaya zaidi nilikuwa juu na hata vile nilivyoanguka nilianguka vibaya baada ya kupoteza fahamu.

Hivyo baada ya huduma ya kwanza niliweza kuwa vizuri palepale uwanjani na baada ya pale nikapelekwa hospitali na matibabu nimepata mazuri na saa 4 asubuhi niliweza kuruhusiwa. Kwa sasa naendelea na matibabu.

Hali yangu inazidi kutengemaa nimebakiwa na maumivu ya nyuma ya kichwa hivyo naendelea na matibabu. Madaktri wanaendelea kunihudumia  zaidi ili niweze kurudi katika hali yangu ya kawaida,” alisema Manula

Kipa huyo alisema kuwa wanaomba mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla kuwaombea waweze kufanya vizuri katika mechi hiyo.

“Nachoweza kuwaambia ni kwamba waendelee kutuombea ili tuweze kupambana na kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Manula.

SOMA NA HII  KOCHA SIMBA: NAMJUA VIZURI IBENGE, NINAJIAMINI