Home Azam FC KOCHA AZAM :- TUNATAKA POINTI TATU ZA IHEFU LEO

KOCHA AZAM :- TUNATAKA POINTI TATU ZA IHEFU LEO


Kocha msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati amesema mchezo wao wa leo dhidi ya Ihefu utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kushinda.

Bahati alisema anajua Ihefu itawakabili kwa hasira baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Biashara United, lakini wamejipanga kukabiliana nao.

“Tunacheza kesho (leo) na Ihefu itakuwa si mechi rahisi kwa sababu wapinzani wetu wanapambana kujinasua kutoka nafasi za chini, lakini pia wametoka kupoteza mchezo uliopita hivyo utaona ni jinsi gani mechi itakavyokuwa ngumu.

“Tunahitaji kutafuta pointi tatu ili kuongeza katika hesabu zetu kwenye msimamo wa ligi. Tunatakiwa kupambana kwa hali yoyote ili kuhakikisha tunashinda nyumbani,” alisema Vivier.

Azam itamkosa nyota wake hatari, Prince Dube, ambaye ana maumivu ya misuli ya paja aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui. Mzimbabwe huyo anatarajia kukaa nje ya uwanja kati ya wiki moja hadi mbili nje ya uwanja.

Kocha wa Ihefu, Zubery Katwila alisema hana tatizo na kiwango ca timu yake lakini jambo linalomuumiza ni jinsi walivyopoteza pointi sita baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo.

Mchezo mwingine leo utakuwa kati ya KMC itakayokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting, utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

SOMA NA HII  HIZI HAPA KLABU 10 ZENYE THAMANI ZAIDI AFRIKA MASHARIKI...CHAMA LAKO NAMBA NGAPI?