Home Simba SC MO DEWJI AWAWEKEA WACHEZAJI WA SIMBA SC MILIONI 200 MEZANI ZA KUIUA...

MO DEWJI AWAWEKEA WACHEZAJI WA SIMBA SC MILIONI 200 MEZANI ZA KUIUA EL MERREIKH KWAO


SIMBA inapaa leo kuwafuata El Merreikh ya Sudan katika mchezo wao wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, huku kocha wa Wekundu hao, Didier Gomes, akisema: “Tulieni nawafahamu vizuri hawa.“

Gomes ambaye ameiongoza Simba katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa walizoshinda kibabe ugenini dhidi ya AS Vita na nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri, amesema mechi itakuwa ngumu lakini ushindi ndio lengo namba moja.

“Tunakwenda kucheza na timu ambayo naifahamu vizuri, tumeandaa mbinu nyingi za kwenda kukabiliana nao ili kuhakikisha tunapata pointi nyingine ugenini ingawa tunatambua si jambo rahisi,” alisema na kuongeza:

“Tumefanya maandalizi ya kutosha kulingana na ambavyo tumewaona wapinzani wetu. Tutatumia udhaifu wao kuwazidi ili kufanya vizuri na ninaamini itakuwa hivyo.

“Wamepoteza mechi mbili, moja nyumbani kwao na nyingine ugenini, hili litaongeza ugumu wa mechi yetu, watataka kupata ushindi wa kwanza, tupo tayari kwa hilo na tutapambana nao,” alisema kocha huyo Mfaransa.

Simba inahakikisha hainasi katika mtego wowote utakaowavurugia mipango yao ya kupata pointi tatu ugenini hivyo imetanguliza jeshi la kwenda kuchonga njia kabla ya timu haijatua mjini Omdurman kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa wikiendi hii.

Jana  Jumanne wanawatanguliza watu wawili, ili kuweka mazingira sawa kama hoteli, usafiri, chakula, uwanja wa mazoezi pamoja na mambo mengine.

Gazeti la Mwanaspoti linajua watu hao wawili watakaotangulia ni Mratibu wa timu, Abbas Selemani ambaye atakwenda kutafuta hoteli ambayo timu itafikia, usafiri, uwanja wa mazoezi na mwingine ambaye atakuwa naye ni mpishi, Samuel Cyprian.

Msafara wa Simba utaongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez akiwa sambamba na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, akiwamo Zacharia Hanspoppe na mshauri wa masuala ya kiufundi Crescentius Magori.

MILIONI 200 TENA

Katika hatua nyingine uongozi wa Simba, chini ya bilionea kijana Mohammed ‘Mo’ Dewji umewaahidi wachezaji wao mkwanja Sh200 milioni kama motisha iwapo wataifunga timu hiyo.

Hii ni mara ya tatu kwa uongozi wa Simba kuahidi kiasi hicho cha pesa kwa wachezaji na tayari wamepandishwa mzuka baada ya wachezaji hao kuvuta Sh400 milioni kutokana na ushindi wa mechi zao mbili na AS Vita na Al Ahly kila mmoja akipata chake.

SOMA NA HII  ISHU YA JEZI MPYA ...SIMBA WAIBUKA NA HOJA HII TENA..WATAJA MUDA NA MAHALI ZITAKAPOPATIKANA...

Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema maandalizi ya timu yanakwenda vizuri na ratiba itakwenda kama ilivyopangwa.

HOMA YA LUIS

Vitu vikubwa vilivyofanywa na kiungo wa ushambuliaji wa Simba, Luis Miquissone katika mechi za Ligi ya Mabingwa msimu huu zimemfanya kuwa gumzo kila kona.

Bao lake kali la juhudi binafsi alilofunga dhidi, Al Ahly Februari 23 jijini Dar es Salaam, limewafanya wapinzani wao El Merreikh kukeshea video za Simba kuangalia namna ya kumdhibiti staa huyo na wenzake kina Clatous Chama, ambaye pasi yake ya mwisho ndiyo iliyompa fursa Konde Boy kufunga bao lililowazamisha Ahly.

Ushindi katika mechi ya ugenini Sudan, utawafanya Simba kutanguliza mguu mmoja kwenye robo-fainali kwani itafikisha pointi 9 na itabakisha kazi ya kusaka pointi mbili katika mechi zao tatu za zijazo – mbili za nyumbani .dhidi ya El Merreikh na AS Vita na moja ya mwisho dhidi ya Ahly, Misri.