Home Yanga SC ZAHERA : SARPONG HANA SHIDA..SHIDA IKO KWA KAZE NA WENZAKE

ZAHERA : SARPONG HANA SHIDA..SHIDA IKO KWA KAZE NA WENZAKE


Kocha wa zamani wa Yanga SC, Mwinyi Zahera amesema kuwa anawashangaa watu wanaomponda mshambuliaji  raia wa Ghana anayeichezea Yanga SC Michael Sarpong, kwani mchezaji huyo ni mzuri ila shida ipo kwa kocha wake.

Sarpong aliyejiunga na Yanga SC  mwanzoni mwa msimu huu wa 2020/21 akitokea klabu ya SC Rayon  ya nchini Rwanda amekuwa akikosolewa na wachambuzi wa soka  pamoja  na mashabiki wa Yanga SC kwa kushindwa kuonyesha makali ya kufunga magoli kwenye mechi za Ligi Kuu.

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Mwinyi Zahera amesema kuwa Sarpong ni mmoja ya washambuliaji wazuri ambao wamekosa msaada wa kimbinu za uchezaji kutoka kwa makocha wake katika benchi la ufundi.

Zahera ambaye sasa ni Mkurugenzi wa ufundi katika klabu ya Gwambina FC inayoshiriki Ligi Kuu, ameongeza kuwa makocha wa Yanga SC wanapaswa kumsaidia Sarpong kuwa bora kwa kumfundisha mbinu za kucheza katika eneo sahihi ndani ya uwanja ili awe bora.

“Ningekuwa Yanga ningeletewa Sarpong ningemsajili haraka na wala nisingechelewa, yule ni mshambuliaji hatari sana hapa, watu hawajui kabisa ubora wa mshambuliaji ndio maana wanamlaumu,” alisema Zahera.

“Kuna namna ya kumfanya mshambuliaji wa namna ile awe anafunga sana na hapo ndipo wanapokosea kuna mbinu ambazo kama kocha unatakiwa kumjenga mshambuliaji.

“Kazi hiyo inatakiwa kufanywa na makocha wake, wanatakiwa kufanya tathimini kupitia video za mechi kwa kuangalia jinsi anavyojituma uwanjani. Lazima utagundua mambo ambayo anakosea, ukishajua unampa mbinu ya jinsi ya kutafuta ‘pozisheni’ na akimbie vipi kulingana na watu wanaomtengenezea mashambulizi.

“Angalia akiwa na mpira hakuna beki ambaye anaweza kuwa na raha, kila wakati beki anaona yupo hatarini, lakini sasa baada ya hapo ndipo kazi ya makocha inatakiwa kufanyika kwa kumwongezea mbinu.”

Amkumbuka Molinga

Aidha, Zahera alimkumbuka mshambuliaji wake wa zamani David Molinga ‘Falcao’, akisema kazi kama hiyo ya kumboresha mshambuliaji aliwahi kuifanya kwa Molinga na akawa mfungaji mzuri.

“Wakati Molinga anakuja wengi hawakuamini kama ni mshambuliaji mzuri, lakini tukamrekebisha akatisha.”

SOMA NA HII  MTAMBO WA MABAO WA YANGA KUTUA LEO