Home Simba SC SIMBA SC WAKOMBA BILIONI 2.7 ZA CAF

SIMBA SC WAKOMBA BILIONI 2.7 ZA CAF


MAFANIKIO ya Simba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, yameifanya iwe timu ya Tanzania iliyovuna kitita kikubwa cha fedha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) huku ikizipiga bao nyingine zilizopata fursa ya kupeperusha bendera ya nchi.

Simba ndani ya kipindi cha miaka hiyo mitano, imevuna kiasi cha zaidi ya Sh 2.7 bilioni (Dola 1.2 milioni) kutokana na hatua ilizofikia kwenye mashindano ya klabu ya Caf, ikifuatiwa na Taifa Stars, Yanga, Namungo, Ngorongoro Heroes pamoja na Serengeti Boys.

Akaunti za Simba zilianza kunona mwaka 2019 pale walipovuna kiasi cha Dola 650,000 (Sh 1.54 bilioni) kutoka Caf kwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu wa 2018/2019 ambayo walitolewa na TP Mazembe ya DR Congo kwa kichapo cha jumla cha mabao 4-1.

Baada ya kutoka patupu msimu uliopita, Simba kwa mara nyingine ina uhakika wa kuvuna kiasi cha Dola 550,000 (Sh 1.26 bilioni) kutoka Caf baada ya kutinga hatua ya makundi ya ligi hiyo msimu huu ambapo hadi sasa wanaongoza kundi A wakiwa na pointi sita dhidi ya timu za AS Vita Club, Al Ahly na Al Merrikh.

Simba wanaweza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya hicho kutoka Caf ikiwa msimu huu watafika hatua za juu za mashindano hayo ambazo ni robo fainali, nusu fainali au fainali.

Kwa mujibu wa mgawanyo wa zawadi za washindi za Caf, timu inayofika hatua ya nusu fainali inapata Dola 875,000 (Sh 2 bilioni), ile inayofika fainali na kufungwa inapata Dola 1.25 milioni (Sh 2.86 bilioni) wakati bingwa wa mashindano hayo anavuna Dola 2.5 milioni (Sh 5.7 bilioni) kutoka shirikisho hilo lenye dhamana ya kusimamia, kuendesha na kuongoza shughuli za mpira wa miguu barani Afrika.

Timu ya Tanzania inayofuatia kwa kuvuna kiasi kikubwa cha fedha kutoka Caf ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita ni Stars ambayo imekomba Dola 675,000 (Sh 1.5 bilioni) kutokana na ushiriki na nafasi ilizomaliza kwenye nafasi mbalimbali.

Kiasi kikubwa cha fedha, Stars ilikipata baada ya kumaliza ikiwa ya mwisho kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) yaliyofanyika mwaka 2019 huko Misri ambako ilipata kifuta jasho cha Dola 475,000 (Sh 1.09 bilioni) pia ikavuna Dola 200,000 (Sh 457.4 milioni) kwa kumaliza nafasi ya tatu hatua ya makundi.

Yanga iko nafasi ya tatu kwenye orodha ya timu za Tanzania zilizopata fedha nyingi kutoka Caf kama zawadi za ushiriki wa mashindano mbalimbali.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita, Yanga imekusanya Dola 440,000 (Sh 1 bilioni) ambazo zote imezipatia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako ilitinga hatua ya makundi mara mbili tofauti ambazo ni mwaka 2016 na 2018.

SOMA NA HII  SIMBA YAIBIGA MKWARA WA KIBABE WYDAD

Bahati mbaya kwa Yanga, walipofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016 na kushika nafasi ya mwisho, timu iliyomaliza mkiani ilikuwa ikipewa Dola 165,000 (Sh 377 milioni).

Lakini walikuja kukutana na neema ya mabadiliko mapya ya viwango vya zawadi yaliyofanywa na Caf mwaka 2017, kwa kuvuna Dola 275,000 (Sh 628.9 milioni) kwa kumaliza mkiani katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018.

Kwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Namungo FC imejihakikishia kitita cha Dola 275,000 (Sh 629.9 milioni) kinachoifanya ishike nafasi ya nne kwa upande wa timu za Tanzania ingawa kinaweza kuongezeka ikiwa itafika mbali zaidi katika mashindano hayo.

Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ yenyewe imevuna kiasi cha Dola 100,000 (Sh 228.7 milioni) kwa kumaliza ikiwa imeshika mkia kwenye Fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zinazoendelea huko Mauritania.

Inayoshika nafasi ya sita ni timu ya vijana ya umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo mwaka 2019 ilishika mkia kwenye hatua ya makundi ya fainali za Afrika na kuvuna kiasi cha Dola 50,000 (Sh 114 milioni) na sasa imeshajihakikishia kupata kitita kama hicho tena au zaidi kwa kitendo chake cha kufuzu Fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika huko Morocco mwezi huu.

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha anasema kuwa kitendo cha timu za Tanzania kushiriki mashindano makubwa na kufanya vizuri sio tu kinazipa fedha bali pia ni chachu ya maendeleo ya soka letu.

“Mashindano kama hayo yanasaidia wachezaji kujiweka sokoni na kujitengeneza fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, yanawapa uzoefu wachezaji, makocha, viongozi na hata mashabiki lakini pia yanaitangaza nchi.

Leo hii ni jambo lililo wazi kwamba Tanzania inazidi kuzungumzwa na kujulikana katika nchi mbalimbali za nje na ndani ya bara la Afrika kutokana na ushiriki na mafanikio ya timu zetu kwenye mashindano ya kimataifa,” anasema Kashasha.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lameck Nyambaya anasema kufanikiwa kwa timu za Tanzania ni jambo la kujivunia kwa nchi nzima.

“Kwa sasa soka la nchi yetu limepiga hatua na juhudi zinazofanyika zikiendelea kuungwa mkono na kila Mtanzania, hapana shaka timu zetu zitapata mafanikio makubwa zaidi ya haya.

“Kama nchi tunatakiwa tuungane kwa pamoja kuhakikisha timu zetu zinakuwa zinafanya vizuri katika kila mashindano zinazoshiriki kwa faida ya nchi,” anasema.