Home Habari za michezo SIMBA YAIBIGA MKWARA WA KIBABE WYDAD

SIMBA YAIBIGA MKWARA WA KIBABE WYDAD

Wakati Simba ikijiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, beki wa Wydad Casablanca ya Morocco, Arsene Zola amekiri Mnyama ana mabadiliko makubwa kiufundi ambayo yanawatia hofu.

Katika mchezo wa kwanza Wydad kwenye uwanja wa nyumbani ilikuwa na wakati mgumu kuikabili Simba ambayo ilichezea kichapo cha bao 1-0, ushindi walioupata dakika za lala salama.

Simba ina rekodi mbaya ya kutolewa na Wydad kwa mikwaju penalti 4-3 msimu uliopita, hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya michezo yote miwili waliyocheza kila mmoja kushinda bao 1-0 nyumbani kwake.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia simu, Zola alisema hakucheza mechi iliyopita baada ya kupata maumivu ya mgongo wakiwa kwenye maandalizi ila wasiwasi wake juu ya kiwango cha Simba ulitimia baada ya wapinzani wao kuonyesha mabadiliko makubwa katika mechi yao hiyo ya kwanza.

Zola alisema Simba licha kupoteza lakini walionyesha mabadiliko makubwa na ilihitaji uzoefu wao tu kuimaliza mechi kwani kwa pande zote mbili hicho ndio kilichohitajika maana wote walikuwa bora.

β€œKilichotupa hofu zaidi ni uwepo Benchikha kwani ninamfahamu tangu alipokuwa anaifundisha RS Berkane ni kocha ambaye ana mabadiliko makubwa ya mbinu na ameanza kuibadilisha timu hiyo na ikipunguza makosa mengi.

β€œKwa kiwango kile cha Simba tunajua kwamba mchezo wao wa marudiano utakuwa mgumu zaidi lakini kwa kuwa tumeshinda mechi ya kwanza imeturudishia morali ya kupambana na kuweka malengo ya ushindi ugenini,” alisema Zola.

Kocha huyo akiwa na RS Berkane mwaka 2022, alikutana na Wydad mara tatu akianza kwa kufungwa 2-0, mechi ya ligi iliyopigwa Oktoba 2022, lakini akawaonyesha ubabe wake kwa kuwafunga mara mbili mfululizo akianza na kushinda 2-0 katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Agosti 27 kisha kuwachapa tena 2-0, Septemba 10, 2022 kwenye fainali ya CAF Super Cup na kubeba ndoo hiyo kubwa Afrika mbele yao.

Simba iliyopo kundi B inashika nafasi ya mwisho kwa pointi mbili chini ya Benchikja, itakuwa na dakika 90 za kujitetea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi hii kuanzia saa 10:00 jioni ikiwa ni mchezo wa nne wa kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SOMA NA HII  BAADA YA KUIONA SIMBA ILIVYOCHEZWA BOTSWANA..EDO KUMWEMBE AGUNA KISHA AFUNGUKA HAYA