HAJI Manara, Ofisa Habari wa Simba amesema kuwa kuna umuhimu wa watani zao wa jadi Yanga kukubali kwamba ni lazima wajiimarishe kwenye uongozi kabla ya kuanza kufikiria mafanikio ya haraka.
Kwa sasa Yanga imefuta makocha wawili ndani ya msimu mmoja ambapo ilianza na Zlatko Krmpotic ambaye aliongoza timu hiyo kwenye mechi tano, alishinda nne na sare moja akafutwa kazi.
Machi 7, Cedric Kaze ambaye alikuwa mrithi wa mikoba ya Zlatko naye alichimbishwa akiwa ameongoza kwenye mechi 18 za ligi, alishinda 10, sare saba na kichapo mechi moja.
Tayari Yanga imemtangaza Juma Mwambusi kuwa kocha wa Yanga wakati wakiendelea na mchakato wa kumsaka kocha mpya ambaye ataendelea na timu kwa mzunguko wa pili ambao unakaribia kumeguka.
Pia Manara amempa pole Kaze kwa kufutwa kazi kwa kumwambia kwamba ni maisha ya soka.
Manara amesema:”Shida yenu kubwa mnataka kushindana na Simba ambayo misingi ya kitimu ishajengwa kitambo. Hamkubali kuwa Simba ni bora maradufu ya timu yenu kwa sasa.
“Hamkubali kuwa tuna management very strong, (Uongozi imara) kuwazidi mara laki, hamjawahi kuelewa, hamjawa bado na uongozi wa kushindana na bodi ya Simba.
“Pia mmekosa kiongozi au mtu kama Haji anayeweza kutoka katika public, (watu) kuwatuliza mashabiki pale hali inapokuwa tete, na hayo yote hayawezekani kufanywa katika muda mfupi kama mnavyoaminishana huko kwenu.
“Pepo tunaitaka lakini haipatikani bila kufa. Hebu shikeni haya maneno toka kwa mtu msiyempenda, siku moja yaweza kuwastiri.
“Kubalini kuwa chini yetu kwa sasa kisha mtengeneze timu na msiamini sana redio na headlines zinazowaaminisha nyie ni bora.
“Kubwa rudini nyuma mvute kasi ya kutufikia tulipo Kwa speed ya mwanariadha, hapo mlipo kukimbia kwa kushindana na Simba hamtaweza hadi kiyama.
“Mnasajili wachezaji wasiopungua ishirini wapya kila mwaka, hii haipo kokote duniani, mbaya zaidi mnaanza kuwapamba hata kabla ya kuingia uwanjani, mnawapokea kifalme ilhali hata utumwa hawastahili,”