Home Ligi Kuu UBABE NDANI YA UWANJA USIPEWE NAFASI, UNATIBUA LADHA YA MPIRA

UBABE NDANI YA UWANJA USIPEWE NAFASI, UNATIBUA LADHA YA MPIRA


 MATUKIO mabaya ambayo yanatokea uwanjani kwa sasa yanazidi kushamiri kila iitwapo leo. Hali hii ni mbaya na inapaswa kuanza kufanyiwa kazi na wachezaji wenyewe.


Ikiwa wachezaji watakubali kwamba mpira ni vita basi kwao kila mchezo ambao watakuwa wanacheza watakuwa wanapigana mabuti mwanzo mwisho.

Usalama wa mchezaji uwanjani unalindwa na mchezaji wa timu pinzani pamoja na timu ambayo anacheza. Ikiwa hakuna ambaye atakuwa anajali italeta matatizo makubwa.

Kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Tanzania Prisons ulitembezwa mpira wa kibabe ndani ya dakika 90. Nguvu kubwa na kila mchezaji akiwa anatafuta mbinu ya kutoka.

Kuna kijana anaitwa Mzamiru Yassin alikutana na balaa la kukutana na teke la Jumanne Elifadhili ambaye anacheza ndani ya Prisons.

Achana na Mzamiru, Shomari Kapombe alikutana na sekeseke la hatari mwendo wa mabuti na kuvutwa mkono. Sawa ikiwa ushindi utakuwa unatafutwa kwa namna hii uwanjani hakuna afya kwenye soka letu huu ni mfumo mbaya kwa wachezaji.

Sio mechi ya Simba na Prisons pekee, mchezo wa Azam FC na Mbeya City nao ulitawala matukio ya ubabe na nguvu nyingi uwanjani.

Prince Dube alikuwa kwenye wakati mgumu kuhimili presha za wapinzani wake muda wote. Pia mpaka sasa nyota wao Yahya Zayd yupo nje ya uwanja na yote ni sababu ya matumizi ya nguvu nyingi.

Kwa mwendo huu ambao tunakwenda nao ikiwa wachezaji hawataamua kubadilika basi mzunguko wa pili unaweza kuwa na wachezaji wengi watakaokuwa benchi kwa sababu ya majeraha.

Ipo wazi kwamba kazi ya mchezaji ni kucheza mpira pale anapopata majeraha ina maana anakuwa nje ya uwanja kwa muda na hili litafanya ashindwe kuendelea kutimiza majukumu yake.

Jikumbushe pia mchezo wa ligi uliowakutanisha Biashara United na Ruvu Shooting ni aina ya mechi ambayo ilikuwa na presha muda wote. Wachezaji kugongana ni jambo la kawaida lakini inapozidi ni hatari.

Ukiweka kando wachezaji, mashabiki nao kwa sasa ni wababe mwanzo mwisho uwanjani katika kushangilia na kusapoti timu zao.

SOMA NA HII  VPL:MBEYA CITY 0-0YANGA

Mashabiki wa Simba ambao wamekuwa wakisifika kwa ustaarabu nao wapo kwenye orodha ya mashabiki wakorofi wakiwa kwenye majukumu yao.


Hawajaanza msimu huu kumbuka kwamba zama za Patick Aussems, Uwanja wa Kirumba baada ya timu yao kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC walimrushia makopo ya chupa kocha kwa hasira.

Wameendelea na kasumba yao ya ukorofi kwa kumpiga na makopo ya chupa pamoja na matunda Jumanne Elifadhili baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu alipomchezea faulo Mzamiru.

Bado ulimwengu wa soka hauhitaji ubabe wala kesi za namna hii. Muhimu mashabiki wawe watulivu na subira katika kuzipa sapoti timu zao.

Mashabiki wa Yanga nao pia wamekuwa wakikumbwa na matatizo hayo ya kurusha chupa kwa waamuzi pale wanaposhindwa kwenda sawa na kasi ya mpira.

Wameweza kupewa adhabu mara kwa mara na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) jambo ambalo limeanza kuwapa funzo kidogo ila hawaeleweki hawa dakika moja mbele wanabadilika.

Kila mchezaji anapenda kuona timu yake ikipata matokeo chanya iwe ni Mohamed Hussein wa Simba hata Idd Seleman wa Azam FC wazawa hawa wote wamekuwa wakipambana kwa ajili ya kuzipa matokeo chanya timu zao.

Kupambana kwa akili na mbinu kunahitajika ila mabavu yanaboa na kupoteza ile ladha ya mpira na kufanya kila mtu awe na hofu.

Kasumba hii imekuwa ikiwasumbua hata wageni pia, kumbuka msimu uliopita mabuti ya Pascal Wawa kwa Ditram Nchimbi.

Kumbuka kwamba Carlos Carlinhos alimpiga ngumi mchezaji wa Ken Gold hata Perfect Chikwende naye alimpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United.

Jambo la msingi kila mchezaji awe mlinzi wa mwenzake.