Home Yanga SC KAPITISHA MWAKA NCHIMBI BILA KUFUNGA, SAWA, LAKINI TUSIISHIE KUMCHEKA

KAPITISHA MWAKA NCHIMBI BILA KUFUNGA, SAWA, LAKINI TUSIISHIE KUMCHEKA

 

MSHAMBULIAJI  Ditram Nchimbi ‘Duma’ wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, amefikisha mwaka mmoja bila kufunga bao ikiwa inaamanisha kwamba siku 365 na zaidi zimekatika mazima.

Yote yamekuja kwa sababu Nchimbi ni mshambuliaji wa kati na imezoeleka kazi ya mshambuliaji ni kufunga mabao bila ya kujali kafungaje. Kitendo cha kukaa mwaka mzima kama mshambuliaji bila kufunga kimeshtua wengi nikiwemo mimi mwenyewe.

Japokuwa kuna muda hubadilishiwa majukumu na kuchezeshwa pembeni, lakini hilo haliondoi jukumu lake mama kwamba yeye ni mshambuliaji asilia na kitu pekee cha kufurahisha watu ni kufunga mabao ndiyo maana baada ya muda huo bila kufunga watu wameibuka huku wengine wakicheka na kubeza juu ya uwezo wa mshambuliaji huyu.

Vyovyote vile ambavyo straika huyo atachukulia kitu muhimu zaidi ambacho anatakiwa kutambua kwamba ana mzigo wa kufanya kwa ajili ya kuwaziba midomo hawa ambao wameibuka na kumnyooshea vidole kwa sasa kwa kufanya kazi nzuri ikiwemo ya kufunga.

Lakini kwangu nina mtazamo tofauti na wengi ambao wanamkejeli au kumcheka straika huyo badala yake nataka tutazame suala hilo kama taifa kwa ujumla.

Kwa nini nasemea taifa ni kwamba wakati ambao tunamcheka Nchimbi kutokana na rekodi hizo kutokuwa nzuri kwake je ni nani ambaye mshambuliaji mzawa ambaye tunamtegemea hasa kwa wakati huu?

Nasema hivyo kwa sababu kila nikitazama mastraika wetu wa hapa nyumbani simuoni hata mmoja ambaye unaweza kusema huyu ni mkali na ambaye ana muendelezo wa kufanya vizuri kwa miaka na miaka.

Kama utazama na kuibuka na straika ambaye ni mkali kwa hapa nyumbani basi ni John Bocco pekee na nje ya hapo hakuna ambaye anaweza kusimama kidete na kupambana na mastraika wengine wa nje ambao wanasajiliwa.

Namtaja Bocco kwa sababu ndiye mshambuliaji pekee wa hapa nchini ambaye amekaa kwenye mstari kwa zaidi ya misimu 10 na anaifanya kazi yake japokuwa amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Tazama kwa misimu ya kati waliibuka mastraika waliofanya vizuri akina Salim Aiyee na Ramadhan Kapera lakini baada ya muda wamepotea na hawasikiki kabisa kwenye soka la hapa nyumbani.

SOMA NA HII  KISA MECHI NA WANIGERIA DAR....CAF WASHUSHA RUNGU ZITO YANGA....

Tunachotakiwa kutambua kwamba tatizo siyo kumcheka Nchimbi kutofunga ila kuelewa kama taifa tumeshindwa kuwa wazuri katika kuzalisha na kuwatunza washambuliaji wetu wazawa.

Hili tatizo ndilo ambalo linatakiwa kushughulikiwa kwa sasa na klabu, wadau pamoja na wote ambao wanasimamia soka letu la hapa nyumbani kuona wanaibua vipaji vipya vya washambuliaji ambao watakuja kufanya mapinduzi katika ligi yetu.

Bila ya kukaa chini na kutafuta majibu ya hiki ambacho kinatusumbua kama taifa tutaendelea kuwa wahesabu wa siku kwa washambuliaji yupi kafikisha siku ngapi bila ya kufunga, kitu ambacho siyo kizuri hata kidogo.

Wakati huu ambao tunacheka na kumnyooshea vidole Nchimbi inatakiwa tuanze kutafuta mwarobaini wa kuwapata washambuliaji wapya ambao watakuja kufanya kazi kwa klabu na taifa kwa siku za mbele.