MECHI dhidi ya AS Vita ndio itaamua hatima ya Simba kucheza robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika au kusubiri kwanza mpaka matokeo ya mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly ambao utakuwa ugenini.
Yamezungumzwa na kuelezwa mengi kuhusu mechi yetu na AS Vita kutokana nasi kupewa nafasi kubwa kuwafunga na kwenda hatua inayofuata.
Katika kolamu zangu mbili za wiki zilizopita nilieleza namna ya ugumu ambao tunakwenda kukutana nao kutokana msimamo wa kundi lilivyo na aina ya matokeo ambayo wameyapata AS Vita.
Sikuishia hapo nilieleza pia namna ambavyo tunatakiwa kuingia kwa nidhamu kubwa katika mechi hii ingawa tutakuwa uwanja wa nyumbani.
Kolamu yangu ya leo ninapenda kuelezea vile ambavyo tutakwenda kuvifanya katika mechi na baada ya dakika 90, kumalizika ndio tutambue kuwa tumefuzu au bado tunakazi nyingine ugenini.
Jambo la kwanza tutacheza kwa nidhamu kubwa katika kushambulia na kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na kuacha hali ya kujiamini kwa kuwa tupo nyumbani na tunaongoza kundi.
Hatutaingia kwa akili ya kucheza kwa kujisahau kuwa tunaweza kushinda kwa kuwa tupo nyumbani na kujivunia matokeo mazuri ambayo tumeyapata katika mechi mbili dhidi ya AS Vita.
Baada ya hilo tutajitahidi kupata mabao ya mapema, hata tukifanikiwa zaidi ndani ya dakika 15 za kipindi cha kwanza ili kuwavuruga kabisa.
Tunajua watakuja na presha ya kutaka ushindi ili kuendelea kuwepo katika mbio za kufuzu hatua ya robo fainali pia kuvunja rekodi ya kuwafunga mara mbili mfululizo.
Kwa maana hiyo kama tukifanikiwa kuwafunga bao la mapema katika dakika za mwanzo maana yake tutakuwa tumewavuruga na kuharibu mipango yao.
Tutaingia katika mechi tukiwa na kiu ya kupata pointi tatu na si moja ili kufikia kile ambacho kipo akilini mwa watu wengi kwa vitendo na si mahesabu ya mdomoni.
Pia hatutakuwa na kumbukumbu yoyote ya mechi mbili ambazo tumecheza na AS Vita kwani ni jambo baya mno katika soka au maisha ya kawaida kuangalia ya nyuma kuliko ambayo unakutana nayo wakati huo.
Ukiwa na akili hiyo hata katika maisha ya kawaida kuwa siku iliyopita ulifanya vizuri katika jambo fulani na likakupa manufaa ukaacha kufanya vyema zaidi wakati uliopo, kamwe hautafanikiwa.
Mpira ndio maisha yetu wachezaji tunatambua na tutaingia katika mechi hiyo kwa ajili ya kusaka mambo kadhaa ikiwamo kuifikisha klabu robo fainali, kujinufaisha wachezaji binafsi na taifa.
Tumepanga kuweka rekodi nyingine ya kufuzu hatua ya robo fainali katika vipindi viwili vilivyokaribiana, jambo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa ni gumu.
Ukiachana na hilo kutakuwa na rekodi mbalimbali ikiwemo kwenda robo fainali kwa kuwafunga AS Vita katika mechi za mwisho kwenye awamu zote mbili.
Kutokana na aina ya mechi ilivyo hayo ndio malengo ambayo tutaingia nayo katika mchezo huo na tunataka kuyafanya yote ili yakitimia tuwe tumeua ndege wawili kwa jiwe moja.
Kwa maoni kuhusu safu hii tuma ujumbe mfupi kwa meseji ya kawaida au Whatsapp kwenda namba 0658-376-417