HEMED Seleman,’Morocco’ Kocha Mkuu wa Namungo FC amesema kuwa watapambana kupata chochote kwenye mchezo wao wa mwisho wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi dhidi ya Pyramids FC ya Misri.
Juzi, ikiwa Uwanja wa Mkapa ilikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca ambapo ni Illias Haddad aliyeanza kupachika bao la kuongoza dakika ya 9, Fabrice Ngoma alipachika la pili dakika ya 14 na msumari wa mwisho ulipachikwa na Zakaria Habti dakika ya 36 na kuwafanya wawakilishi hao wa Tanzania kuyeyusha pointi tatu.
Akizungumza na soka la bongo, Morocco alisema kuwa kikubwa ambacho kimekuwa kikiwapa shida kwenye mechi za kimataifa ni uwezo wa wachezaji wake kukosa uzoefu pamoja na uchovu jambo ambalo atalifanyia kazi kuelekea kwenye mchezo wake wa mwisho.
“Tumekuwa kwenye mwendelezo mbaya wa kushindwa kupata matokeo na ipo wazi kwamba hatuna ule uzoefu kwenye mechi za kimataifa pamoja na utofauti wa ubora wa wachezaji ambao tunakutana nao.
“Kwenye mchezo wetu wa mwisho tutapambana kupata chochote ili kumaliza tukiwa na pointi kwa kuwa safari yetu imekwisha tayari hivyo tunaingia camp, (kambini) kwa ajili ya maandalizi yetu,” amesema.
Mchezo ujao kwa Namungo ni dhidi ya Pyramids unatarajiwa kuchezwa Aprili 28 ambapo kwenye kundi D, Pyramids ipo nafasi ya pili na pointi 9 huku Namungo ikiwa haina pointi nafasi ya nne kwa kuwa mechi zote 5 ilipoteza.
Ilipokutana na Pyramids mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Machi 17, ubao ulisoma Namungo 0-2 Pyramids hivyo utakuwa ni mchezo wa kisasi kwa Namungo ugenini kwenye Uwanja wa 30 June.