KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya PSG, Neymar amesema kwasasa anafanya mazungumzo na klabu yake hiyo na kusisitiza kuwa anajisikia vizuri na mwenye furaha tele.
Neymar ameyasema hayo wakati akiwa anazungumza na wanahabari kuhusu maandalizi ya mchezo wa leo Aprili 28, 2021 wa nusu fainali ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya utakaochezwa saa 4:00 usiku dhidi ya Manchester City kwenye uwanja wa Pac de Prince nchini Ufaransa.
Neymar amesema.“Nimekwisha liongelea hili mchezo uliopita, nina furaha sana hapa Paris. Ninafanya mazungumzo na PSG, nina jisikia vizuri na nina furaha”.
Katika kuzungumzia jinsi mchezo huo utakavyokuwa na malengo ya PSG msimu huu, Neymar amesema:
“Utakuwa ni mchezo mgumu, Manchester City ni timu kubwa na PSG ni miongoni mwa timu kubwa Duniani. Mwaka uliopita tulifika fainali, mwaka huu tuna imani tutashinda kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
“Tunapaswa kuendelea kucheza kwa juhudi na kucheza vizuri kama kweli tunataka kubeba kombe ambalo tunalitaka kwa udi na uvumba.”
Mara ya mwisho PSG kukutana na Manchester City, PSG ilitolewa kwenye hatua ya robo fainali miaka mitano iliyopita.
Walipotinga fainali walipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich Agosti 23, 2020 jambo ambalo lilimfanya nyota huyo amwage machozi, wametinga hatua ya nusu fainali kwa kuwavua ubingwa mabingwa watetezi.