Home Yanga SC HILI LINAWEZA KUMSUMBUA MWAMBUSI

HILI LINAWEZA KUMSUMBUA MWAMBUSI


HOFU kubwa ya kikosi cha Yanga ni kwamba baada ya mechi tatu zijazo, watakuwa katika nafasi gani. Maana sasa wako katika nafasi ya kwanza kwa maana ya vinara wa Ligi Kuu Bara.

Yanga wamecheza mechi 23 na kukusanya jumla ya ponti 50. Pointi hizo zinawafanya wao kuwa kileleni lakini hofu ni walio katika nafasi ya pili, watani wao Simba ambao wana pointi 46 baada ya kucheza mechi 20.

Ukiangalia tofauti ya pointi nne tu na michezo ni mitatu, kama Simba atashinda yote, atakuwa ameiacha Yanga mbali. Kwa Yanga hili ni jambo linalowachanganya.

Kwamba baada ya muda mfupi wataondoka kileleni na kama ni hivyo wataing’oa vipi tena Simba kileleni na hasa kuhusiana na suala la kiwango cha wenyewe Simba itakuwaje na hakuna ubishi kwa aina ya uchezaji wao, wako vizuri zaidi.

Hii presha inatembea ndani ya viungo vya Yanga na kuifanya wakati mwingine kujilazimisha kufanya vitu nje ya mwendo wake ambayo ni hatari zaidi.

Kwa Kocha wa muda, Juma Mwambusi yeye lazima atakuwa na presha kwa kuwa amekichukua kikosi kikiwa kimecheza mechi sita na kupata sare nne, kikashinda moja na kupoteza moja. Hiki ndicho kilimfanya Kocha Cedric Kaze raia wa Burundi atupiwe virago vyake.

Kwake Mwambusi lazima atakuwa anataka kuanza ligi na ushindi lakini ukweli, inawezekana kukawa na ugumu katika hili kwa kuwa bahati mbaya ligi imelazimika kusimama kwa muda mrefu kutokana na mapumziko yaliyotokana na msiba wa Rais John Pombe Joseph Magufuli.

Timu inapokaa muda mrefu bila ya kucheza, hata kama inaendelea na mazoezi, bado itakosa match mentality na match fitness. Maana yake wakati kikosi cha Mwambusi kinarejea katika ligi, basi kitakuwa ndio kinajijenga.

Yanga kuanza kujijenga kutokana na mechi zinazoendelea kunaweza kutengeneza presha zaidi. Mfano angalia mechi ya kwanza dhidi ya KMC, haiwezi kuwa mechi nyepesi na unakumbuka mara ya mwisho wawili hao walipokutana, KMC walilalama kuonewa.

Angalia baada ya hapo Yanga wanakwenda kukutana na Biashara United, timu ambayo unaweza kusema ukiacha timu za Dar es Salaam, inaonekana kuwa ndio timu imara zaidi inayotokea nje ya mkoa huo kwa timu za Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  MASHABIKI WA YANGA HAPO KIGALI SIO POA

Kama itatokea Yanga wataanza vizuri mechi dhidi ya KMC kwa kuwa ushindi, basi hii itakuwa msaada mkubwa sana kwenda katika mwendelezo wa mechi nyingi kwa kuwa itaamsha morali na ile hali ya hamu ya kushinda itaendelea.

Bahati waliyoipata Yanga, katika mechi zao nne zinazifuatia, zote hawatalazimika kusafiri, zote watakuwa nyumbani na hii ni nafasi kubwa kwa kusimama.

Ikitokea pia Yanga wakafanikiwa kushinda mechi zao zote nne zinazofuatia. Basi watakuwa na nafasi ya kufanya vema zaidi katika mechi nyingine zinazofuatia ingawa si uhakika wa asilimia mia itakuwa hivyo.

Mwambusi inabidi ajiandae, kwamba kwa kuwa mechi ndio zinaanza na wao walisimama kwa muda mrefu na bahati mbaya hakuna hata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki kwenye viwanja vya ushindani, basi litamsumbua.

Ikitokea limemsumbua jambo hili, lazima ajipange na kupambana. Mashabiki na mambo ya ufundi, ni wachache wao sana. Wengi wanachotaka kama ilivyo kwa mashabiki wengi, wanataka kushinda na hakuna mjadala.

Mashabiki wanachojua ni timu yao kushinda na unaona ndio maana nilisema Mwambusi ameingia wakati mbaya. Kwamba mashabiki watakacholenga ni kwamba, kwa kuwa Mwambusi amerejea kama kocha mpya, watataka kuona timu yao inashinda tu.

Presha kwa Yanga haiwezi kushuka leo au mapema, lazima kuwe na subira kutoka katika kila pande kwamba kuibadilisha hii hali, katikati yake lazima kuwe na maumivu.

Credit – Saleh Jembe