Home Yanga SC YANGA IMLIPE TAMBWE MAPEMA HALAFU TUHAMIE HUKU

YANGA IMLIPE TAMBWE MAPEMA HALAFU TUHAMIE HUKU


DENI la Yanga dhidi ya mshambuliaji wake wa zamani, Amissi Tambwe linazidi kupaa kutokana na kwamba halilipwi au halijalipwa kwa wakati.

 Tambwe anaidai Yanga takribani dola 21,000 (zaidi ya Sh 48,696,600), hii ni baada ya kupeleka madai yake katika Mahakama ya Usuluhishi (CAS) na mwisho yakatoka majibu kwamba zile fedha za usajili na baadhi yake ya fedha za mishahara na gharama za kuendesha kesi, Yanga illipe.

Kwa mujibu wa Tambwe mwenyewe, anaamini fedha hizo zitakuwa zimefikia dola 22,000 au zaidi kwa kuwa muda umepita na Yanga bado hawajalitekeleza hilo.

Deni hilo linaweza kuendelea kuwa kubwa kila kukicha hasa kama Yanga wataendelea kuchelewa kulilipa kwa kuwa sheria ziko wazi. Kuna kipindi, Yanga itaingia katika wakati mgumu kwani inaweza kuzuiwa kusajili.

Ukiangalia Yanga ni ileile kweli lakini chanzo cha deni hilo kinaanzia nyuma lakini upande mwingine viongozi walio madarakani wanahusika pia.

Kwa Yanga kutoa fedha kama hizo zinazotakiwa kwa wakati huu, haliwezi kwua jambo jepesi. Na huenda linaweza likawa jambo gumu zaidi kwa kuwa wadhamini wanaweza wakawa hawahusiki sana maana wangependa kujihusisha na mambo wanayoona yanaipeleka klabu hiyo mbele na si madeni ya nyuma.

Kuna mambo mengi yanawakabiri kipindi hiki na wangependa kuona wanayakamilisha au wanayafanya kwa ufasaha kwa kuwa presha inazidi kuwa kubwa kutokana na mwendo wa wapinzani wao, mfano Simba na hata Azam FC.

Maana yake, wanajikuta wamewekeza zaidi katika nguvu nyingi katika mwendo wao kipindi hiki lakini wanashindwa kujua, mambo haya ya madeni yanaweza kuja kuwa tatizo kubwa zaidi hapo baadaye.

Ugumu wake ni kwamba kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo deni linazidi kuongezeka. Litaendelea kuongezeka na kutengeneza hasara kubwa zaidi kwa kuwa hata hapo awali, halikuwa kubwa hivi lakini baada ya kesi likapanda.

Maana yake, baadaye kama linazidi kuongezeka, Yanga itajikuta inalipa hadi dola 30,000 au zaidi. Na utaona, hata kabla ya kesi, kulikuwa na hali ya kulipuuzia jambo hilo hadi ilipofikia kesi kwisha.

SOMA NA HII  KOCHA YANGA:MUUNGANIKO KWELI BADO, SIWEZI KUDANGANYA

Sasa Yanga wasiendelee kurudia kosa linalofanana na lililowafanya wao kuingia kwenye hasara hii. Badala yake, wamlipe Tambwe fedha zake lakini ikiwezekana kufanya mawawasiliano ya kibinadamu dhidi ya wengine wanaowadai.

Kuwa salama, Yanga lazima wajitahidi kumlipa Tambwe, lazima wakubali kuzungumza na wengine ambao wanawadai na kuangalia njia sahihi na bora kuhakikisha wanalipa madeni yao hasa ya wachezaji ambao waliachana nao.

Baada ya kufanya hivyo, Yanga watakuwa na nafasi ya kufungua ukurasa mpya na baada ya hapo wataendesha mambo yao kitaalamu na weledi zaidi na kuepukana na kesi kama hizi ambazo wakati mwingine zitakuwa zinawatoa njiani bila ya sababu za msingi.

Nasema inawatoa njiani kwa kuwa wanajikuta wanaanza kupambana na deni wakati huu si wakati mwafaka kwao kuanza kufikira namna ya kulipa deni badala ya kufikiria njia sahihi za kuisaidia timu kupambana na mwisho kupata mafanikio makubwa.

Wakati fulani, wachezaji wa kigeni na hata wa hapa nyumbani walikuwa wakilalama kudhulumiwa fedha zao na klabu mbalimbali lakini na hasa hizi kubwa na hakukuwa na kesi nyingi.

Wakati huu unaona watu wamebadilika, wachezaji wa kigeni ndio usiseme, watu wanajitambua na wanajua njia zipi za kudai haki zao.

Badala ya wale wanaodai haki zao kuchukuliwa kama maadui, badala yake klabu zijifunze na kuliepuka jambo hili maana wachezaji kama unazungumza nao vizuri na ikiwezekana wakaanza kulipwa taratibu, nao ni wanadamu lazima watakuwa waelewa na mwisho mnamaliza salama.