Home epl MBWANA SAMATTA ANAPITIA KIPINDI KIGUMU, LAZIMA APAMBANE

MBWANA SAMATTA ANAPITIA KIPINDI KIGUMU, LAZIMA APAMBANE

 

MSHAMBULIAJI  Mbwana Samatta kwa michezo 11 ya karibuni aliyocheza katika timu yake ya Fenerbahce hajafanikiwa kufunga goli baadhi ya michezo akianza na mingine akitokea benchi.
 
Akiwa na klabu hiyo amecheza jumla ya michezo 22 ndani ya michezo hiyo amefunga magoli manne tu, si takwimu nzuri kwa mshambuliaji kama Samatta ambaye alifanya makubwa akiwa na kikosi cha KRC Genk kabla ya kutimkia Aston Villa.
 
Ni kipindi kigumu kwa Samatta, hana maisha mazuri ya kimpira kwa siku za karibuni, hata ushiriki wake katika upatikanaji wa goli ndani ya timu ni asilimia saba tu.
 
Kwa takwimu hizi ni ngumu kumuona Samatta akibaki pale Fernabahce baada ya mkopo wake kumalizika mwezi  Juni 2021.
 
Na pia maisha yake akirudi Aston Villa siyaoni sana, tayari pale wana mshambuliaji Ollie Watkins anayefanya vizuri sana kwa sasa, ni ngumu mwalimu kushawishika kumrudisha Samatta labda aamue kubadilika na kuhakikisha anapambania namba yake ndani ya Villa.
 
Je Samatta ubora wake umeshuka au timu aliyopo mfumo wake haumbebi Samatta, yote yanaweza kuwa majibu lakini kwa namna tofauti.
 
Ni ukweli usio hitaji maelezo mengi kuwa Samatta kwa sasa anapita kipindi kigumu, hata uchezaji wake ndani ya timu ya taifa si bora sana kama mwanzo, ana ari ya kutaka kufunga lakini mambo hayaonekani kwenda vizuri.
 
Sababu ya mfumo wa timu pia nadhani ni sahihi, ndani ya ligi hiyo ya uturuki mchezaji anayeongoza kwa magoli anaitwa Aron Pozzi anayecheza Klabu ya Hatayspor, yeye amefunga magoli 18.
 
Lakini ndani ya Klabu ya Fenerbahce anayeongoza kwa magoli ni Mame, aliyefunga goli tano, yani goli moja mbele ya mbwana Sammatta.
 
Kwa takwimu hizo unaona kabisa timu haifanyi vizuri linapokuja swala la kuwalisha mipira washambuliaji katika nafasi sahihi.
 
Ipi nafasi ya Samatta kwa sasa, nadhani ndo kitu muhimu kwake, kwa aina ya uchezaji wa Samatta naona bado atahitajika na baadhi ya timu barani ulaya.
Kwa sasa anachohitaji ni kupambana kurudisha kujiamini kwake mbele ya goli, kelele za mashabiki wa Fernabahce kwake zimekuwa nyingi azitumie tu kuongeza kasi, kama ilivyo kauli mbiu yake ya haina kufeli.
Bado ninaamini katika uwezo wake ni moja ya wachezaji bora na washambuliaji wa kiwango bora. Huenda majeraha aliyoyapata yalichangia kumrudisha nyuma kwa kiasi kikubwa lakini hilo anapaswa kulichukua kama changamoto kwa yeye kurudi kwenye ubora wa yule Samatta wa KRC Genk.
 

SOMA NA HII  BRUNO AKOMALIA ISHU YA KUPIGA PENALTI