LICHA ya kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali ya Europa League kwa kutolewa na Villarreal ambayo inanolewa na Kocha Mkuu, Unai Emery, Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta anaamini kwamba ataendelea kuwa kwenye timu hiyo kwa msimu ujao.
Arteta anaamini kwamba ana uwezo wa kufanya vizuri wakati ujao na kuwapa kile ambacho wanakihitaji mashabiki wa Arsenal.
Uongozi wa Arsenal imeelezwa kuwa upo tayari kumpa nafasi nyingine kocha huyo mwenye miaka 39 kuendelea kukinoa kikosi hicho.
Ila habari zimeeleza kuwa nafasi ya Arteta kubaki ndani ya kikosi hicho inategemea nafasi ambayo atamaliza kwenye Ligi Kuu England kwani mabosi hawataona shida kumfukuza kocha huyo ili kumpata kocha mwingine.
Alipoulizwa kuhusu nafasi yake ndani ya timu hiyo Arteta ambaye alishinda taji la FA msimu uliopita alisema:”Ndio, ninadhani kikosi kinahitaji mabadiliko. Tayari kuna mabadiliko ambayo tumeanza kuyafanya Desemba, jambo ambalo halikufanywa nyuma kuna mambo ambayo yanakwenda kubadilika nina amini uongozi utafanya hivyo nami nina amini bado nipo,” .