KIUNGO wa Klabu ya Yanga ambaye ni mkongwe ndani ya Ligi Kuu Bara kwa sasa anapata tabu kupata namba kikosi cha kwanza tofauti na zamani ambapo alikuwa ni chaguo la kwanza.
Nyota huyo pia ameweza kucheza katika timu zote mbili kubwa ambazo ni Simba na Yanga na aliweza kutwaa taji la ligi alipokuwa ndani ya Simba na kikosi hicho kilitinga hatua ya robo fainali.
Msimu huu wa 2020/21 akiwa ndani ya Yanga iliyocheza jumla ya mechi 27 Niyonzima ameweza kucheza jumla ya mechi 12 na kutumia dakika 371.
Tabu anayopata ni kwamba kwenye mechi hizo 12 hajapata bahati ya kuyeyusha dakika zote 90 pia hajafunga bao wala kutengeneza pasi ya bao.
Mechi zake ilikuwa namna hii:-Mbeya City, dk 69, Kagera Sugar, dk 7, Coastal Union, dk 45, Polisi Tanzania, dk 59, KMC 9, Ruvu Shooting, 19, Mwadui dk 30, Ihefu, dk 14, Kagera Sugar, dk 16, Polisi Tanzania, dk 77, Biashara United dk 14, Azam FC, dk 12.
Kuhusu nafasi yake ndani ya kikosi cha Yanga ambacho kinanolewa na Kocha Mkuu, Nassredine Nabi Niyonzima alisema kuwa anamuachia mwalimu ila kazi yake yeye ni kucheza.
“Mimi ni mchezaji na jukumu la kuanza ama kutoanza hiyo ni kazi ya mwalimu. Nikipata nafasi ninatimiza majukumu yangu kwa ajili ya kuisaidia timu yangu, hivyo kuanza ama kutokuanza hilo lipo mikononi mwa mwalimu,” alisema.