Home Ligi Kuu KUAHIRISHWA SIMBA V YANGA, SAA 2 ZILIVYOWAZIDI NGUVU VIONGOZI YANGA

KUAHIRISHWA SIMBA V YANGA, SAA 2 ZILIVYOWAZIDI NGUVU VIONGOZI YANGA


Na Saleh Ally

KUNA kanuni, kuna sheria na hizi zinapaswa kufuatwa lakini mbele yake kuna busara ambayo inapaswa kutumika juu ya hizi kwa lengo jema kabisa.


Achana na ile kauli ya sheria zimeundwa ili zivunjwe, lakini unaweza kusema busara imekuwepo ili kuokoa kila kinachoonekana kinakwenda mrama na kuizidi nguvu sheria au kanuni ambazo zinakuwa zinaongoza jambo fulani.


Sheria zinaundwa na wanadamu, lengo ni kukiongoza kitu kwa kusimamia utaratibu ulio sahihi na kunakuwa na wale ambao wamekabidhiwa kuusimamia utaratibu huo, kuna wakati hata wao hukosea.


Uongozi wa Yanga, juzi umepitisha uamuzi wa kuitoa timu yao uwanjani wakieleza namna Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuvunja kanuni ya ubadilishwaji wa kanuni ya kubadilishwa kwa muda wa mechi ambayo inaagiza angalau saa 24 kabla ya muda

sahihi wa mechi. Yanga wameamua kufuata kanuni, wameamua kutoa timu uwanjani baada ya kupewa taarifa mapema taarifa ya kwamba mechi itaahirishwa lakini haikuwa ndani ya saa 24.


Katika hali ya kawaida kulikuwa na mambo ya muhimu kujifikiria kuhusiana na suala hili. Na mimi na wewe twende tuliangalie namna hii, kwamba kweli uongozi wa Yanga umefuata kanuni, hawana kosa. Lakini tujiulize walijifikiria madhara ya kutovumilia saa 2 tu zilizokuwa zimesogezwa mbele?


Tujiulize, uongozi wa Yanga kama ungeacha timu yake icheze baada ya saa 2 mbele, nini ambacho ingepoteza kwa timu kusubiri saa mbili. Maana hakukuwa na suala la kuahirisha badala yake kusogezwa mbele (delay) kwa saa 2 tu mbele.


Saa hizo mbili halikuwa agizo la TPLB wala TFF, lilikuwa ni agizo la Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Jiulize, kuna mawasiliano yoyote viongozi wa Yanga walifanya na wizara kutaka kujua undani wa suala lililowalazimisha wao kuchukua uamuzi huo?



Si vibaya tukisema wizara na Yanga ni wale wanaofanya kazi sehemu moja, maana yake ni rahisi kufungua mashauriano kuhusiana na jambo fulani ambalo linakuwa limetokea kwa lengo la kujenga au kufanya jambo fulani. Walijaribu hilo kwa kuwa tayari TPLB waliwaeleza kwamba lilikuwa ni agizo la wizara ambayo ndiyo Serikali.


Haya yote hayakufanyika kwa kuwa uongozi wa Yanga huenda waliliangalia suala hili kishabiki tu na binafsi naona lilikuwa linawezekana kujadiliwa kwa udogo, halafu kuangalia kifanyike kipi kilicho sahihi kuhakikisha mechi inachezwa kwa kuwa Yanga walishafanya maandalizi yao na hadi wanapeleka timu uwanjani walikuwa tayari kwa mchezo, saa 2 mbele zingefanya maandalizi waliyokuwa nayo yayeyuke?

SOMA NA HII  FUPA LA IHEFU FC NI NOMA KWELI


Kubwa zaidi ambalo tunapaswa kumshukuru Mungu ni kuhusiana na kwamba watu walitoka angalau salama uwanjani na hakukuwa na maafa na hili huenda lingekuwa la kwanza kabisa kwa viongozi wa Yanga na wakaribu wao kulifikiria tena kwa kiwango cha uongozi na si viongozi kuwa mashabiki.


Narudia, saa 2 mbele zingeharibu vipi maandalizi ambayo Yanga walikuwa wamefanya kwa ajili ya mechi hiyo? Watu tayari walikuwa uwanjani na kama Yanga wanatoa timu, lingetokea suala la hasira na wao kuamua kufanya vurugu, kwa idadi ya watu zaidi ya 40,000, nani angeweza kuwazuia? Yangetokea maafa nani alipaswa kulaumiwa?


Bila shaka aliyeamuru timu kutoka uwanjani, bila ya kufanya mashauriano na mmoja wa wadau wao ambao ni TPLB na TFF ambao lazima waliwaeleza kuwa ni Serikali na wao wangewafikia!

Najiuliza, kwamba viongozi wa Yanga walishindwa kuona kunaweza kuwa na maafa na uvumilivu wa saa 2 mbele ndiyo uliwashinda, au uliharibu maandalizi yapi kwa kikosi chao na vizuri zaidi, wasingecheza peke yao. Maana hata wapinzani wao Simba pia walilazimika kusubiri hizo saa 2 kama walivyokuwa wameelezwa. 


Sasa tofauti ni nini hapo? Viongozi Yanga walifikiria usumbufu wa fedha za waliokuwa wameingia uwanjani? Au waliona haliwahusu kwa kuwa wenyeji wa mechi ni Simba?

Lakini wanajua hata mashabiki wao pia walilipa? Bado hawakujiuliza watu wametoka mbali kwenda kuiunga Yanga mkono pale Benjamin Mkapa.

Achana na yule aliyesafiri kwa miguu kutoka Kigoma, wako wale ambao waliingia uwanjani tangu saa 4 asubuhi wakaisubiri Yanga kwa zaidi ya saa 7 na yenyewe ikashindwa kusubiri saa 2 mbele!

Lazima tukubali, kuna shida kubwa hapa kwa viongozi wa Yanga na hakika walishindwakuonyesha busara na weledi wa uongozi kama wazazi na wakaamua mambo kishabiki, jambo ambalo huenda lingeweza kuleta madhara makubwa.Tumeona Polisi walilazimika kupambana na baadhi


ya mashabiki waliokuwa wakitaka kurudishiwa fedha zao, wakarusha mabomu ya machozi na hakukuwa na madhara makubwa. Hili ni jambo la kushukuru lakini kuwasisitiza viongozi Yanga, wakati mwingine vizuri kutumia ukomavu, uzoefu, weledi na busara ikawaongoza kwa nia njema kabisa kwa kuwa wakati mwingine, madhara yanaweza kuwa makubwa na mwisho tukaishia kujilaumu kwa kuamua mambo kwa mihemko.