Home Ligi Kuu KWA MKAPA HAPATABIRIKI, HAWA NI WAKALI WA KUTUPIA

KWA MKAPA HAPATABIRIKI, HAWA NI WAKALI WA KUTUPIA


KUNYANYUKA kwa mashabiki wa Simba na Yanga kushangilia bao Mei 8 kutategemea jitihada za miguu 22 ya wanaume ambayo itakuwa inapambana kusaka pointi tatu ndani ya Uwanja wa Mkapa.

Dabi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ile vita ya kusaka taji la Ligi Kuu Bara ambapo yule atakayeshinda atachochea moto mbio za kuelekea kwenye ubingwa jambo linalofanya kwa Mkapa kushindwe kutabirika mapema.

Mabingwa watetezi wao wana pointi 61 ambao ni Simba nafasi yao ni ya kwanza na Yanga nafasi ya pili na pointi zao 57. Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mechi zao zote za ligi ambazo jumla ni 25 Uwanja wa Mkapa, timu hizo zimefunga jumla 52 na kufungwa jumla ya mabao 15.

Kwa namna yoyote ile huenda kuna mtu atapasuka ama watatoshana nguvu kama mchezo wao wa mzunguko wa kwanza ulivyokuwa Yanga 1-1 Simba, tusubiri na tuone dakika 90 zitaongea hebu cheki rekodi zao kwa msimu huu Uwanja wa Mkapa, Spoti Xtra inakuletea namna hii:-

Simba

Mechi 12 za ligi ambazo ni dakika 1,080 imeshinda mechi 9 ambazo ni dakika 810 sare 3 dakika 270 na haijapoteza kwa Mkapa.

Mabao ya kufunga

Imefunga mabao 33 ina wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 32 na kufungwa mabao matano ikiwa na wastani wa kuokota bao moja kila baada ya dakika 216.

Mechi zake kwa Mkapa

Simba 4-0 Biashara United , Simba 4-0 Ihefu, Simba 3-0 Gwambina, Yanga 1-1 Simba, Simba 2-0 Polisi Tanzania, Simba 1-0 KMC, Simba 4-0 Ihefu, Simba 2-2 Azam FC, Simba 3-0 JKT Tanzania, Simba 1-1 Tanzania Prisons, Simba 5-0 Mtibwa Sugar na Simba 3-1 Dodoma Jiji

Wakali wa kucheka na nyavu

Meddie Kagere ni namba moja kwa kuwa na ushikaji na nyavu kwa Mkapa. Akiwa na jumla ya mabao 11, ni mabao 8 ameyafunga kwa Mkapa na matatu kafunga nje ya uwanja huo.

 Ni Biashara United, Gwambina, Azam FC, KMC hawa waliokota nyavuni bao mojamoja na mabao mawili mbele ya Ihefu na Mtibwa Sugar.

SOMA NA HII  GWAMBINA FC YAKOMAA NA KUBAKI LIGI KUU BARA

Chris Mugalu ana jumla ya mabao 8, sita alitupia kwa Mkapa, alitupia mbele ya Biashara United, Gwambina FC, Ihefu FC na JKT Tanzania ilikuwa mwendo wa mojamoja na Dodoma Jiji aliwatungua mabao mawili.

 Clatous Chama ametupia mabao 7, mabao matano alitupia kwa Mkapa ambapo mabao mawili mbele ya Biashara United, mabao mawili mbele ya Polisi Tanzania na bao moja mbele ya Mtibwa Sugar.

 

Yanga

Mechi 13 za ligi ambazo ni dakika 1,170 imeshinda mechi 7 ambazo ni dakika 630 sare 5 ndani ya dakika 450 na kupoteza mechi moja.

Mabao yao

Mabao ya kufunga ni 19 ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 61 ya kufungwa ni 10 sawa na wastani wa kuokota mpira kwenye nyavu zao kila baada ya dakika 117.


Mechi za Yanga

Yanga 1-1 Namungo, Yanga 1-1 Prisons, Yanga 1-0 Mbeya City, Yanga 1-1 Simba, Yanga 1-0 JKT Tanzania, Yanga 3-0 Coastal Union, Yanga 2-1 Ruvu Shooting, Yanga 3-3 Kagera Sugar,Yanga 1-0 Mtibwa Sugar, Yanga 1-1 KMC, Yanga 1-0 Biashara United, Yanga 3-1 Biashara United, Yanga 0-1 Azam FC.

Wakali wa kutupia kwa Mkapa

Yacouba Songne mwenye mabao 6 matatu aliyatupia kwa Mkapa, aliwatungua Coastal Union wakati Yanga ikishinda mabao 3-0, aliwafunga KMC wakati ubao ukisoma Yanga 1-1 KMC na aliwatungua Biashara United.

Carlos Carlinhos kibindoni ana mabao matatu na yote ameyatupia Uwanja wa Mkapa. Bao moja mbele ya Mtibwa Sugar, bao moja mbele ya Namungo FC na bao moja Coastal Union.

Michael Sarpong, ana mabao manne, alitupia moja mbele ya Tanzania Prisons,aliwatungua bao moja Simba kwa mkwaju wa penalti na Ruvu Shooting bao moja.