Home Simba SC MO DEWJI AWAPIGIA ‘SALUTI’ GOMES NA MATOLA

MO DEWJI AWAPIGIA ‘SALUTI’ GOMES NA MATOLA

 


Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ameonekana kuvutiwa na kazi ambayo inafanywa na benchi la ufundi la timu hiyo.

Mo Dewji kupitia mitandao yake ya kijamii aliandika ujumbe ambao uliambatana na picha ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Picha hiyo walikuwepo, Kocha mkuu, Didier Gomes na msaidizi wake, Selemani Matola, Kocha wa viungo, Adel Zrane, Kocha wa makipa, Milton na Meneja Patrick Rweyemamu.

Mo Dewji katika ujumbe wake aliandika “Sisi sote mashabiki wa Simba tunafuraha sana kuona timu yetu inaendelea kufanya vizuri,” ameandika na kuongezea;

“Makocha wetu wapendwa mpo nyuma ya mafanikio ya timu.

“Tunashukuru kwa uthubutu wenu na kujitoa kwenu na tuna imani kwamba mtaendelea kuisaidia Simba kufanya vizuri zaidi,”

Simba ikiwa chini ya Mo Dewji amefanya vizuri katika mashindano mengi yale ya ndani pamoja na nje ya nchi.

Miongoni mwa mafanikio hapa ndani wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo na kuchukua mataji mengine.

Miongoni mwa mataji mengine waliochukua ni kombe la Shirikisho (ASFC) pamoja na Ngao ya hisani.

Katika mashindano ya kimataifa chini ya Mo Dewji miongoni mwa mafanikio ambayo Simba wameyapata, wamefika katika hatua ya robo fainali Ligi ya mabingwa mara mbili.

Msimu huu Simba wamefika katika robo fainali ila kikosi chao kutokana na uwekezajj uliofanywa na Mo Dewji wanaweza kusonga katika hatua inayofuata.

Simba chini ya Mo Dewji wameboresha kikosi chao kwa kufanya usajili wa wachezaji wa maana kama Clatous Chama, Luis Miquissone, Chriss Mugalu, Meddie Kagere, Aishi Manula, John Bocco na wengineo wengi.

Mbali ya mafanikio hayo chini ya Mo Dewji Simba imebadilisha makocha wakuu kwa sababu mbalimbali.

Kocha wa kwanza kubadilishwa ni Mcameroon Joseph Omog, baada ya hapo akaja Pierre Lechantre aliyefanya kazi pamoja na Masoud Djuma.

Baada ya muda makocha hao waliondoka kwa vipindi tofauti na walikuja Patrick Aussems na Denis Kitambi ambao nao waliondoka.

SOMA NA HII  KUMBE SVEN ALIBWAGA MANYANGA KIMYAKIMYA, SIMBA HAWAKUTAKA KUACHANA NAYE

Baada ya kuondoka makocha hao alikuja, Sven Vandenbroeck akiwa pamoja na Selemani Matola.

Siku moja baada ya Sven kuivusha Simba katika hatua ya makundi, aliondoka na nafasi yake ilichukuliwa na Didier Gomes ambaye yupo mpaka sasa.