DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa anatambua ubora wa kiungo wake Bernard Morrison ila ataangalia namna ya kuweza kuanza naye kwenye mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.
Mei 8, Simba itawakaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Mchezo wa kwanza walipokutana ubao ulisoma Yanga 1-1 Simba huku watupiaji wakiwa ni Michael Sarpong kwa upande wa Yanga na Joash Onyango kwa upande wa Simba.
Katika mchezo huo Morrison alikosekana kwa kuwa alikuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu baada ya kupigana na mchezaji wa Ruvu Shooting, Juma Nyoso.
Gomes amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Yanga ni muhimu kwao kushinda na anaamini kuwa itakuwa kazi ngumu kujua kama Morrison ataanza ama la kwa kuwa bado kuna muda wa maandalizi.
“Ukimzungumzia Morrison ni aina ya wachezaji wazuri ambao wapo kwenye kikosi, kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga ni suala la kusubiri mambo yatakuaje kwani bado kuna muda wa kujiandaa.
“Ninajua kwamba wengi wanasubiri kuona itakuaje ila tunajiandaa kwa umakini na kufanya mipango iende sawa ili kupata ushindi katika mchezo huo,” .
Nyota huyo alijiunga Simba akitokea Yanga kwa kusaini dili la miaka miwili hivyo anatarajia kukutana na mabosi wake wa zamani.
Mchezo wa mwisho kusimamia Gomes ilikuwa ni ule wa Kombe la Shirikisho ambapo Morrison alianzia benchi na kubadili mchezo pale alipoingia kwa kuwa alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao.
Kwa ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Kagera Sugar mabingwa hao watetezi wa Kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu Bara waliweza kutinga hatua ya robo fainali.
Mchezo wake unaofuata ni dhidi ya Yanga na utakuwa ni mchezo wa kwanza kwake kukaa kwenye benchi kwa kuwa alibeba mikoba ya Sven Vandenbroeck.