Home Simba SC WACHEZAJI WALIOFANYA MAAJABU NDANI YA SIKU 100 ZA GOMES, SIMBA SC

WACHEZAJI WALIOFANYA MAAJABU NDANI YA SIKU 100 ZA GOMES, SIMBA SC


 ITAKAPOFIKA Mei 4, mwaka huu kocha wa Simba SC, Mfaransa Didier Gomes atakuwa amefikisha siku 100, tangu alipoanza kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

Gomes aliyekuja nchini 24, Januari na kuanza kazi siku hiyo hiyo alichukua nafasi kutoka kwa Sven Vandenbroeck aliyeondoka pasipo kutegemewa na wengi.

Katika muda huo ambao Gomes amekuwa na  Simba SC kuna mafanikio mbalimbali ameyapata katika mashindano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwenye mafanikio hayo wachezaji wote wa Simba SC waliopata nafasi ya kucheza kila mmoja alitoa mchango wake kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo.

Gomes akiwa ndani ya Simba SC kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa na kiwango bora kutokana na rekodi zao mbalimbali ambazo wanazo mpaka wakati huu.

Meddie Kagere

Wakati wa Sven, Kagere hakuwa anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara na kuna baadhi ya mechi alikuwa akiingia zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya mchezo kumalizika.

Gomes mara baada ya kufika Simba SC mambo yalibadilika kwa Kagere na straika huyo wa Rwanda akaanza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa awali.

Kagere ameonekana kuwa msaada kwa Gomes kwani mpaka wakati huu ndio kinara wa magoli katika kikosi cha Simba SC akifunga 11.

John Bocco

Amekuwa akipata majeraha ya mara kwa mara ambayo kuna nyakati yanamuweka nje na kukosa mechi nyingi katika mashindano mbalimbali.

Bocco licha ya kupitia changamoto hiyo ameonekana kuwa na mchango mkubwa kwa Gomes, kwani anashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi katika kikosi cha Simba SC.

Bocco amefunga mabao kumi katika Ligi Kuu na kuchangia kuipa timu yake pointi tatu muhimu kama alivyofunga katika mchezo dhidi ya Mwadui bao lake la pekee lililoipa ushindi timu yake.

Chriss Mugalu

Wakati wa Sven, Mugalu alikuwa akipewa nafasi ila mara nyingi alitokea benchi la wachezaji wa akiba lakini wakati huu mambo ni tofauti kwake.

Mugalu mpaka sasa ameingia katika orodha ya nyota waliombeba Gomes kwani amefunga mabao nane na anakuwa mchezaji wa tatu mwenye mabao mengi kwenye kikosi hicho.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo amembeba Gomes si katika mashindano tu, bali hata kwenye Ligi ya Mabingwa alifunga mabao mawili kwenye hatua ya makundi.

SOMA NA HII  ALICHOKISEMA ALLY MAYAI KUHUSU NANI BORA KATI YA PABLO NA NABI...AWATAJA FEI TOTO NA MORRISON...

Clatous Chama

Kiungo fundi na roho ya kikosi cha Simba SC katika kupika mashambulizi, ndiye chanzo cha takribani kila hatari inayojengwa na Simba SC.

Chama katika kikosi cha Simba SC mpaka sasa amevunja rekodi yake ya mabao aliyofunga msimu uliopita pamoja na pasi za mwisho.

Msimu uliopita Chama alitoa asisti kumi na kufunga mabao mawili, lakini msimu huu kufikia sasa baada ya mechi 25 ametengeneza asisti 13 na kufunga magoli saba.

Kiungo huyo raia wa Zambia amechangia mabao 20, kwenye kikosi cha Simba SC amekuwa akionyesha makali yake mpaka katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Luis Miquissone

Miongoni mwa nyota ambao chini ya Gomes wamefaya vizuri ni Miquissone ambaye katika Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya makundi ndio mchezaji aliyefunga mabao mengi.

Katika makundi amefunga mabao matatu, wakati katika ligi ameifungia timu yake mabao saba na kuwa katika orodha ya wachezaji wenye mabao mengi ndani ya timu hiyo

Miquissone amekuwa mchezaji hatari katika kikosi cha Simba SC na kwenye mashindano yote amefanya vizuri.

Aishi Manula

Kipa chaguo la kwanza katika kikosi cha Simba SC, ameonyesha kiwango bora kiasi kwamba katika kila mechi timu hiyo imekuwa kwenye mikono salama.

Usalama huo wa Simba SC ni kutokana na kiwango cha Manula kuimarika zaidi chini ya Gomes na kupunguza makosa yake kama kufungwa magoli ya mbali, magoli ya frii-kiki na mipira ya kona au krosi.

Joash Onyango

Katika kikosi cha Simba SC, Gomes amekuwa akifanya mabadiliko ya mara kwa mara, lakini si kwa beki wa kati, Onyango ambaye ametumika katika mechi nyingi.

Beki huyu raia wa Kenya, ameonyesha kiwango bora msimu huu pengine tofauti na ambavyo ilitarajiwa wakati anasajiliwa kutoka Gor Mahia ya Kenya. Wengi walimfanyia dhihaka wakimtania kuwa ni mzee.

Kebehi hizi zilizidi baada ya kuachwa kwa kasi ya umeme na winga wa Yanga, Tuisila Kisinda, lakini tangu hapo amethibitisha kuwa yeye ni β€˜nusu mtu nusu chuma’.

Mbali ya kujenga ukuta wa chuma, Onyango ameifungia Simba SC bao moja na asisti moja.