Home Uncategorized CORONA IMETUSAHAULISHA KABISA KUHUSIANA NA MAISHA YA VIJANA NA SOKA

CORONA IMETUSAHAULISHA KABISA KUHUSIANA NA MAISHA YA VIJANA NA SOKA




NA SALEH ALLY
HAKUNA ubishi kweli mambo yanamebadilika sana na yanakwenda nje ya utaratibu ambao tumekuwa tukienda nao kwa miaka yote.


Kinachotokea sasa kuhusiana na maambukizi ya Covid 19 imekuwa ni mpya, ngeni nay a kushangaza kwa kila mmoja wetu na hakuna aliyeitarajia.


Ndio maana unaona hata wale wenye nguvu ambao mwanzo walibeza, kwa sasa wanaonekana kuchanganyikiwa kwa kuwa hakikuwa kitu ambacho walikiratajia.


Katika michezo, kama ilivyo karibu kila sehemu ya dunia hii, mambo yameharibika  kabisa. Gumzo sasa limekuwa ni kuhusiana na ligi kubwa za Ulaya na ligi za nchi husika kuwa zitarejea lini.


Hamu ya kuona mechi zikichezwa tena ndio imekuwa kubwa. Kutokana na hali hiyo ni nadra kwa asilimia 99 kusikia watu wakijadili kuhusiana na vijana ambao nao wanaingia katika janja hili la Corona. 

Shule zimefungwa, wako nyumbani kwa kuwa ni hatari. Michezo nayo imesimamishwa hawawezi kushiriki kwa kuwa ni hatari lakini nani anazungumza kuahusiana na watoto na vijana na wanatakiwa kufanya nini ili kupita kipindi hiki kigumu.

Angalia kwa wewe mtu mzima namna ambavyo kwa kuwa utaratibu umelazimika kupindishwa kutokana na hali halisi iliyopo, wenyewe inakuwaje? Jiulize wewe mtu mzima unaweza wakati fulani “kukontroo” mambo yako na kujiweka sawa, nani anawaweka vijana hawa katika wakati wanaoweza kurejea wakiwa sahihi.


Maana wana ndoto, walikuwa wanajua baada ya muda fulani watafanya hivi na vile. Walijua baada ya muda watafikia sehemu fulani kwa mazungumza ya sasa na ni kama vile kila kitu kimesimama na sasa ndio mwisho.

Matumaini yanazungumzwa kwa kipindi kidogo sana na mazungumza yote ni kuhusiana na wakubwa na ligi zao n ahata ile hali ya kuanza mazoezi tena ilivyoanza, unaona mabadiliko ni kwamba wakubwa wanaendelea kufanya mazoezi kwa program kadhaa na si vijana au watoto. Ukweli ni kwamba wamesahaulika si Tanzania, inawezekana sehemu nyingi sana duniani lakini huu ndio wakati wa kukumbuka na kukumbushana.

Kutokana na kwamba wale wachezaji wa timu kubwa wao ndio tegemeo kwa maana ya biashara yenyewe ya mpira, si vibaya kweli wakawa wanazungumziwa sana.

Pamoja na hivyo, lazima tukumbuke kama mpira ni biashara basi biashara hii ina muendelezo na vijana au watoto wanaochipukia sasa, ndio biashara ya mpira ya baadaye.

Kama hawa watakata tamaa leo na sisi tukakubali hili liendelee maana yake tunatengeneza tatizo la baadaye kwa kuwa itafikia hatua kutakuwa na wachezaji waliokosa kitu fulani wakati fulani.

Wakati huu ni rahisi kijana aliyekuwa anakataliwa kucheza mpira nyumbani kwao naye alikuwa anawashawishi, akaamua kuungana na wazazi wake kwa kuwa anapoteza hamu na kuona ule umuhimu wa mpira.

Hakuna aliye karibu na kuzungumza naye, kumueleza kinachofuatia na nini afanye. Huyu mtu anatakiwa awe anatokea katika mpira ili mtoto kijana aendelee kuona mpira unamjali na baadaye utakuwa msaada baada ya kwisha kwa vita hii ya Corona.
Kama sasa wakati wa shida na watu wa mpira hawaoni, unatarajia afanye nini? Hawezi kuwa na Imani kubwa na alipo na ndio maana nasema anaweza kukata tamaa mara moja na kuachana na mpira ambao huenda ungekuwa maisha yake au kwa kipaji chake alichonacho, angeibuka na kuwa shujaa wa taifa siku moja.

Vizuri makocha wapate nafasi ya kuzungumza na vijana hata kwa simu, wakumbushwe na kupewa angalau program za nyumbani, mazoezi yanayoweza kuendelea kuwakumbusha kuwa mpira upo, unaendelea na utaendelea baada ya Corona hivyo hawapaswi kukata tamaa kwa kuwa watu wa mpira wako nao.




SOMA NA HII  MZEE AKILIMALI AMCHANA AJIBU, AMUITA KIRUSI