Home Uncategorized USIOGOPE RAPHAEL DAUD, TOKA KWENYE GIZA LA DAR ES SALAAM

USIOGOPE RAPHAEL DAUD, TOKA KWENYE GIZA LA DAR ES SALAAM



Na Saleh Ally
BOBBY Robson ndiye kocha Mwingereza mwenye heshima kubwa kuliko mwingine yeyote nje ya nchi hiyo kutokana na ubora wa kazi yake akiwa na klabu mbalimbali za Ureno na baadaye Hispania.


Anajulikana alipokuwa akiinoa PSV ya Uholanzi halafu akahamia Ureno ambako alifanya kazi nzuri akiwa na Sporting Lisbon nchini Ureno na baadaye wapinzani wakubwa wa timu hiyo, FC Porto wakamchukua ambako alifanya nao kazi kabla ya kuhamia Hispania ambako alitua FC Barcelona ambayo alifanya nayo kazi kabla ya kurejea Uholanzi kuinoa PSV Eindoven kwa mara nyingine.


Alimalizia kazi yake ya ukocha akiwa na Newcastle na mshambuliaji mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu England hadi sasa, Allan Shearer anasema pamoja na kuwaheshimu makocha wengine lakini heshima kubwa zaidi katika maisha yake ipo kwa Robson.


Moja ya stori za Robson inayonivutia sana ni ile aliyomuambia Romario aliyetaka kutoroka kwenda kushiriki lile tamasha lao la Carnival kwao Brazil, kwamba asifanye hivyo, anachotakiwa amfungie mabao mawili katika mechi iliyokuwa mbele ili ampe ruhusa.


Kwa kuwa mechi ilikuwa muhimu sana, Robson alitaka mtu wa kufunga tu mabao hayo ili ajue atakavyofanya kipindi cha pili. Kweli dakika 45 zikaisha, Romario alishatikiza nyavu mara mbili FC Barcelona ikawa inaongoza halafu yeye akamruhusu aondoke wakati wa mapumziko na tayari alikwenda na begi lake kwenye mechi akiamini atafunga aondoke.


Kocha huyu anasifiwa kwa kuwavumbua akina Ronaldo de Lima kwa maana ya kuwakuza baada ya kuona kipaji lakini ndiye aliyemuibua Kocha Jose Mourinho ambaye awali alikuwa mtafsiri wake pale Barcelona. Anasifika kwa mengi lakini moja ya sifa kubwa ni kuhakikisha kipaji cha mchezaji hakifi sababu ya matakwa ya kocha au makocha.


Mara zote, Robson alikuwa akiwaeleza wachezaji asiotaka kuwatumia na anaamini wana vipaji waondoke zao na wakati mwingine akiwashauri timu bora na sahihi kuichezea. Wengi sana walifanikiwa baada ya kufuata ushauri wake, ndiyo maana ni kocha kipenzi zaidi cha wapenda mpira kuliko mwingine yeyote kwa Waingereza ndani na nje ya nchi hiyo.


Wakati namkumbuka Robson ambaye nilivutiwa sana na kitabu chake wakati nakisoma, nimejikuta namkumbuka kiungo Raphael Daud wa Yanga ambaye sasa yuko gizani.


Kiungo huyu mwenye umbo adimu, kati ya mambo tunayoyasaka kwa shida, mwenye kipaji ambacho wachache wanacho lakini mwenye nidhamu na asiye na makuu, amezama gizani Dar es Salaam.


Nasema Dar es Salaam kwa kuwa alikuwa katika mwanga mng’aavu wakati akiwa Mbeya City akiwa mmoja wa wachezaji waliowapa shida kubwa wapinzani wakiwemo Yanga, Simba, Azam FC na timu nyingine ngumu zilizokutana na Mbeya.


Hata baada ya kuja Yanga, cheche zake zilionekana kwa kiwango kizuri tu. Baadaye ikaanza kuonekana alikuwa hana nafasi kubwa sana lakini kila alipopata nafasi ya kucheza alifanya vizuri na mmoja wa makocha waliompa nafasi kubwa na akaonyesha alichonacho ni George Lwandamina.


Nakumbuka alianza kupotea wakati wa Mwinyi Zahera ambaye huenda hakuvutiwa naye au wakati mwingine nafikiria kocha huyo hakuwa na subira sana au muda mwingi wa kushauri wachezaji kama ilivyo kwa Lwandamina ambaye huwa kocha na mzazi pia aina ya Robson.


Siwezi kukubaliana na mtu yeyote hata wewe msomaji kama utaniambia Raphael uwezo wake umeporomoka au hajiwezi wala siwezi kukubaliana na yeyote kama ataniambia kuwa Raphael hana uwezo wa kucheza katika kikosi hiki cha sasa cha Yanga.


Mfano ukiangalia namba sita, saba ambayo ni ya kuvunja ndani, namba nane, namba 10 au 11 ya kuvunja ndani. Namba zote hizi kweli hawezi kupata nafasi katika kikosi hiki cha Yanga kwa wakati huu?


Ninaamini Raphael amekosa mtu aina ya Robson ambaye anaweza kumtoa gizani na akasema ikiwezekana hata Yanga ondoka.


Kama hachezi, pia nilisikia alitakiwa kupelekwa kwa mkopo akagoma, basi sasa anasubiri nini Yanga na Yanga inamzuia wa nini akiwa anaendelea kukaa benchi na kama hataki kwenda kwa mkopo, waingie makubaliano na ikiwezekana kumuachia aende zake sehemu ambayo kipaji chake kinaweza kuamka tena.


Raphael alishaichezea Taifa Stars, kuitwa kwake timu ya taifa inathibitisha uwezo wake na anaweza kwenda mbele zaidi ya hapo, hivyo asikubali kubaki katika giza la Dar es Salaam na wakati huu wa mapumziko ya lazima kutokana na hofu ya Ugonjwa wa Covid 19, vizuri ukawa muda wake wa kutafakari na kuamua njia sahihi ya kumtoa katika giza zito la Jiji la Dar es Salaam pale Jangwani.




SOMA NA HII  HIZI HAPA DAKIKA 180 ZA MOTO KWA YANGA NA SIMBA KABLA YA MACHI 8