Home Uncategorized NDEMLA NA SIMBA KIMEELEWEKA..AWEKEWA FUNGU LA MILIONI 30 KUSALIA MSIMBAZI

NDEMLA NA SIMBA KIMEELEWEKA..AWEKEWA FUNGU LA MILIONI 30 KUSALIA MSIMBAZI

UONGOZI wa Simba unaendelea kusuka kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao kwa kutafuta wachezaji wa maana kutoka hapa ndani ya Tanzania na nje ya mipaka.

Simba ilianza harakati za kuwabakisha wachezaji wao wanaomaliza mikataba mwisho wa msimu huu ambao ni Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya na Hassan Dilunga ambaye alikuwa akihusishwa kwenda Yanga.

Habari zinasema kwamba Simba wamempa tayari mkataba Ndemla tangu Alhamisi iliyopita saa 5 asubuhi kwenye jengo la Diamond Plaza Posta Jijini Dar es Salaam.

Habari zinasema walikaa kikao cha majadiliano ambacho kilichukua muda wa saa mbili hadi kumalizika saa 7 mchana baina yake na Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa, pamoja na Makatibu Hamis Kisiwa na Dkt. Anord Kashembe.

“Kikao kilichukua muda wa saa mbili na sisi Simba tumeafiki kumpa Ndemla Sh30milioni ili asaini tena, alikubali ila aliomba tumpe siku saba akashauriane na familia yake pamoja na watu wake wa karibu wenye uelewa wa masuala ya kimkataba,” kilidokeza chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Simba.

“Siku hizo saba zitamalizika Ijumaa ya wiki hii na ndio atakuja na majibu kamili kuwa ameshasaini mkataba wetu ambao ameondoka nao tayari, kwani kuna vipengele vya maslahi tumeviongeza katika huo mkataba na kama kutakuwa na jingine lolote atatueleza.

“Nadhani mkataba wetu tulivyouboresha atasaini na tutaendelea kuwa naye misimu miwili mbele kwani bado tunamhitaji katika timu yetu,” kiliongeza chanzo hicho.

Senzo alisema halitakuwa jambo jema kwao kusajili wachezaji wapya bila ya kumalizana na mastaa muhimu waliokuwa nao msimu huu akiwemo kiungo huyo ambaye yeye na Jonas Mkude ndiyo waliodumu na kikosi hicho kwa muda mrefu zaidi kati ya waliopo sasa.

Ndemla mwenyewe alisema; “Unajua baada ya kumaliza kucheza soka watu watakuja kuniuliza nilikuwa nafanya nini kipindi nacheza mpira kwa maana hiyo kila uamuzi ambao nayafanya, nawashirikisha watu wangu wa karibu ambao naamini ni sahihi kwangu.

“Kuhusu masuala ya mkataba wangu kumalizika au nitacheza timu gani hilo kusubiri muda rasmi utafika kila kitu kitafahamika lakini itambulike mimi bado ni mchezaji halali wa Simba,” alisema Ndemla ambaye amekuwa akishinikizwa aondoke akacheze atakakopata namba.

SOMA NA HII  KMC WATIA TIMU RWANDA, TAYARI KUIVAA TP MAZEMBE