Home news FAINAL ASFA: HIVI NDIVYO HISTORIA INAVYOIBEBA SIMBA SC DHIDI YA YANGA

FAINAL ASFA: HIVI NDIVYO HISTORIA INAVYOIBEBA SIMBA SC DHIDI YA YANGA


JULAI 25, kule Kigoma patachimbika. Ndio, Kigoma ni mwisho wa reli, lakini unaambiwa Julai 25 patakuwa ni mwisho wa ubishi, nyodo na tambo wakati miamba miwili ya soka nchini, Yanga na Simba itakapokutana kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC). 

Ushindi wa bao 1-0 iliyopata kila kila timu katika mechi za nusu fainali dhidi ya Biashara United na Azam FC, zimeupa mkoa wa Kigoma mechi hiyo kubwa yenye upekee na hadhi kubwa zaidi katika mchezo wa soka nchini.

Uwanja wa Lake Tanganyika utakaoandaa mchezo huo pasipo shaka yoyote unaingia katika orodha ya viwanja vilivyopo nje ya Dar es Salaam vilivyowahi kuandaa mechi ya timu hizo mbili kubwa na kongwe nchini, walio watani wa jadi.

Kabla ya hapo, viwanja ambavyo vimewahi kupata bahati hiyo nje ya Dar es Salaam ni CCM Kirumba na Nyamagana (Mwanza), Sheikh Amri Abeid Kaluta (Arusha), Jamhuri (Morogoro) na Amaan (Zanzibar), Jamhuri Dodoma na Sokoine Mbeya.

KAZI IPO

Timu hizo zitakutana kwenye fainali hizo huku kila upande ikiwa na morali kubwa na nyota ambao wana uwezo mkubwa wa kuamua mchezo, chini ya makocha Didider Gomes wa Simba na Nasreddin Nabi wa Yanga ambaye moto wake umeanza kuonekana tangu ampokee Cedric Kaze.

Mechi hiyo inakuja ikiwa Simba na Yanga zinakutana wikiendi hii katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara, ambayo awali ilipangwa kufanyika Mei 8, lakini ukaahirishwa, baada ya mchezo wao wa kwanza kuisha kwa sare ya 1-1 katika mechi iliyopigwa, Novemba 7, 2020. 

Pia inakuja ikiwa ni kama miezi zita tu tangu zikitane pia katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Januari 13, 2021, hivyo kufanya mmchezo wa fainali hiyo ya ASFC, itakuwa bab’ kubwa na Wanakigoma utamu wataupata Julai 25.

KISASI HAKIEPUKIKI

Pamoja na heshima ya kutwaa taji, mechi hiyo ni fursa nzuri na muhimu kwa kila timu kulipa kisasi cha matokeo ya nyuma baina yao pindi walipokutana katika mashindano tofauti.

Simba bila shaka watakuwa na kiu ya kulipa kisasi cha kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 na Yanga katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika muda wa kawaida wa mchezo.

Yanga wenyewe kwa upande wao watakuwa na hamu ya kulipa kisasi cha kufungwa mabao 4-1 na Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, Julai mwaka jana.

MZANI UMEBALANSI

Takwimu za mechi tano zilizopita zinatoa taswira ya ugumu wa mechi hiyo ya fainali ambayo itakutanisha timu hizo mbili katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Timu hizo zote kila moja imepata ushindi katika mechi zote tano zilizopita ambayo imecheza huku zikiwa zinakaribiana katika kufumania nyavu na safu ya ulinzi.

Simba imeshinda mechi zake tano zilizopita za mashindano tofauti dhidi ya Azam, Mbeya City, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting na Namungo FC, ikipachika mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Kwa upande wa Yanga, nayo imeshinda mechi zake zote tano zilizopita, mbili dhidi ya Mwadui na nyingine ilizocheza na Biashara United, Ruvu Shooting na JKT Tanzania, ikifumania nyavu mara 11 huku yenyewe ikifungwa mabao manne.

SOMA NA HII  MTIBWA SUGAR YAZITAKA POINTI SITA MAZIMA

REKODI ZAIPA JEURI SIMBA

Simba wana rekodi nzuri ya mechi za fainali wanazokabiliana na Yanga nje ya mkoa wa Dar es Salaam kwani wamefanya vizuri kulinganisha na watani wao.

Achana na fainali ya kwanza ya Kombe la ASFC (enzi hizo kama National Cup) 1974 iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza na ile ya fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 1975 ambazo zote Yanga ilishinda kwa mabao 2-1 na 2-0 mtawalia.

Fainali saba za mashindano tofauti zimekutanisha timu hizo mbili kubwa na kongwe nchini nje ya Dar es Salaam ambapo Simba wameibuka na ushindi mara nyingi kuliko Yanga.

Simba wameibuka na ushindi katika fainali nne ambazo ni ile ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1992 waliposhinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, mwaka 2005 waliposhinda mabao 2-0 kwenye fainali ya Kombe la Tusker iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na mwaka 2007 walipoibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 5-4 katika fainali ya ligi ndogo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro. 

Fainali nyingine ya nje ya Dar es Salaam ambayo Simba iliibuka na ushindi dhidi ya Yanga ni ile ya Kombe la Mapinduzi mwaka 201 waliposhinda 2-0.

Yanga yenyewe imeibuka na ushindi mara tatu. Mara ya kwanza ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Hedex iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mwaka 1996 kwa mabao 2-0, ikaifunga Simba kwa mabao 3-0 katika Uwanja huohuo wa CCM Kirumba katika mechi ya Ngao ya Hisani mwaka 2003 na mwaka huu ikaibuka na ushindi wa penalti 4-3 huko Visiwani Zanzibar kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa katika Uwanja wa Amaan.

WASIKIE WADAU

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anaamini kuchezwa kwa fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) Kigoma kunaweza kuwa chachu ya kuamsha timu, wadau wa mkoa huo ambao burudani za namna hii wamezikosa kwa kipindi kirefu.

“TFF wanatamani kuona Watanzania wote wakifurahia soka, isiwe Dar na mikoa mingine michache mpira ukichezwa miaka nenda miaka rudi, ni jambo zuri kujaribu kuhamasisha mchezo wa mpira wa miguu uchezwe karibu nchi yote, hatutaona timu ya Kigoma ikicheza fainali lakini najua watahamasika ili miaka ijayo wawe na timu Ligi Kuu,” alisema Ulimboka.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mohammed Badru, alisema kilichofanywa na TFF ni kama vile walivyofanya UEFA.

“Nadhani wanataka kila sehemu waufurahie mpira, badala ya mashabiki wa Kigoma kufunga safari ya kuja Dar kwa fainali sasa wamepelekewa kwao, ni jambo zuri sana,” alisema Badru na kuongeza;

“Itapendeza sana kama huu muundo ambao wameutambulisha uendelee hivi hivi lakini tuboreshe sasa viwanja vya mikoani ili kuondoa visingizio kwa timu kushindwa kuonyesha viwango vyao,TFF wakae chini na viongozi wa vyama (CCM) ili kuviboresha.”

Naye Amri Kiemba aliyewahi kufanya makubwa akiwa na Taifa Stars, alisema,”Hii ni moja ya njia ya kujaribu kufufua mikoa ambayo inaonekana ni kama imekufa kisoka, itasaidia sana kukata kiu ya mashabiki ambao kwa kipindi kirefu walikosa fursa ya kuitazama michezo mikubwa kama hii.”