Home Yanga SC YANGA WAMKANA IBRAHIM AJIB MCHANA KWEUPEEEH…

YANGA WAMKANA IBRAHIM AJIB MCHANA KWEUPEEEH…


MASHABIKI wa Yanga wakisikia kuna taarifa za kurejea kwa aliyekuwa nahodha wao wa zamani, Ibrahim Ajibu wanageuka mbogo hawataki kusikia hilo na sasa uongozi wao umeweka bayana msimamo wa hatma ya mshambuliaji huyo kurejea.

Aliyetoa msimamo huo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dominic Albinus na amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti kuwa katika mkoba wake ana majina kadhaa ya wachezaji wapya wa maana wanaotakiwa kusajiliwa msimu ujao, lakini hakuna jina la Ajibu wala mchezaji yeyote kutoka Simba.

Yanga iliwahi kukaribia kuwasaini Shomary Kapombe, John Bocco, Mohamed Hussein, Luis Miquissone na Cletous Chama.

Albinus aliongeza, sio tu kuhusu Ajibu wameondoa kila kitu juu ya uwezekano wa kumsajili mchezaji yeyote kutoka Simba kwa msimu ujao na wana watu wa maana zaidi wanataka kuwaleta.

“Tunasikia tu hizo taarifa na wanachama wanaonekana kuchanganyikiwa kila mmoja akiwa mkali kwa viongozi wenzangu kuhusu huyo Ajibu na hatujajua chanzo chake ni kipi,” alisema Albinus ambaye kamati yake hushirikiana na kamati ya usajili ambayo mmoja wa wajumbe wake ni Injinia Hersi Said ambaye amekuwa akishughulikia mara kwa mara dili za usajili na katika dirisha lililopita mastaa kadhaa aliwafuatia katika nchi zao kuwaleta Jangwani.

Miongoni mwa mastaa hao ni Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda kutoka DR Congo.

“Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, tunafanya usajili tukishirikiana na uongozi wa klabu na wadhamini wetu GSM, lakini naweza kuthibitishia katika majina ya wachezaji tunaowataka hakuna jina la Ajibu na wala halijawahi kujadiliwa katika watu tunaowataka, pia hatuna hata jina moja la mchezaji wa Simba.”

Albinus ambaye kitaaluma ni kocha aliongeza kuwa Yanga hawawezi kumsajili Ajibu ambaye msimu mzima amekuwa akisotea benchi akikosa nafasi ya kucheza katika klabu yake.

“Hatuwezi kumsajili Ajibu kwa historia yake makosa ya namna hiyo hayawezi kufanyika sasa, hajacheza karibu msimu mzima huu, mchezaji wa ndani tutakayemsajili kila mtu atakubali takwimu zake kwa kile ambacho amekifanya ndani ya msimu mmoja unaoisha au zaidi,” alisema.

SOMA NA HII  KISA MECHI YA SIMBA NA WAIVORY...YANGA WASHINDWA KUJIZUIA...WAIBUKA NA HILI JIPYA....

Aliongeza sababu nyingine ambayo hata kama Ajibu angekuwa na kiwango kizuri msimu huu kingemzuia kusajiliwa Yanga ni jinsi alivyoondoka huku wakiwa walimpa heshima kubwa.

“Watu lazima wajue hili, kuna maisha ya kesho kuna namna ambavyo Ajibu aliondoka hapa wengi walikasirishwa hasa ukizingatia klabu, wanachama na mashabiki walimpa heshima kubwa hadi kuwa nahodha lakini alirudi klabu anayoipenda, ni vyema akabaki huko au kwenda klabu zingine zitakazoona anafaa.

“Tutasajili wachezaji bora msimu ujao, ni kazi ambayo tulianza muda mrefu, tunafahamu usajili wakati mwingine ni kama kamari lakini safari hii tutakuwa makini zaidi tunajua shida ya kikosi chetu.

“Umakini hautaishia kwa wachezaji wa ndani pekee, tutakuwa makini pia hata kwa wachezaji wa kigeni na huko mambo yatakuwa magumu zaidi katika kufanya uamuzi, vile vigezo vya ubora wa mchezaji wa kigeni vitafanyiwa kazi kwa utulivu.”

Ajibu anamaliza mkataba Simba mwisho wa msimu huu, hatua ambayo ilizusha uvumi anakaribia kurejea Yanga aliyoitumikia misimu miwili kabla ya kurejea Simba akiwa na kiwango bora.

Aliongeza katika usajili wao ujao, wanafanya kazi kwa kumshirikisha Kocha wao, Nesreddine Nabi kuangalia ubora wa wachezaji.

“Tunaheshimu uwezo wa Ajibu lakini ni vigumu kutetea usajili wake kwa mtu ambaye hajamuona akicheza,” alisema Albinus.