KIKOSI cha Azam FC jana, Julai 7 kiliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba kwenye mchezo wa kirafiki.
Ni Nivere Tigere alipachika bao la kwanza dk 25 na bao la pili lilipachikwa na Bruce Kangwa dk 32 na kuwafanya waweze kwenda mapumziko ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Azam FC 2-0 Pamba.
Kipindi cha pili Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, George Lwandamina iliongeza spidi ya kusaka ushindi ambapo iliwachukua zaidi ya dakika 11 kupachika bao lingine ndani ya kipindi cha pili.
Ilikuwa ni kazi ya kiungo wao mshambuliaji Ayoub Langa ambaye alipachika msumari huo dk ya 56.
Ngoma ilikuwa ngumu kwa Klabu ya Pamba ya Mwanza iliyokuwa na mastaa kama Salum Mlemwa, Said Khamis na Emmanuel Haule kuweza kupata bao la kufuta machozi ndani ya dk 90 kwa kuwa mikono ya Mathias Kigonya kipa namba moja wa Azam FC haikuruhusu hayo yatokee.
Pia Azam FC iliwashushia Pamba FC kikosi kazi kwa kuwawekea ukuta wa chuma ambapo walianza ilikuwa ni Nicolas Wadada pamoja na Yakub Mohamed ambao ni chaguo la kwanza kwa Lwandamina.
Kwenye safu ya ushambuliaji alikuwepo Obrey Chirwa, Mpiana Monzinzi ambao walianza nao pia kikosi cha kwanza.