KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes, amesema anasikitika muda mwingi aliopoteza kutazama video za michezo iliyopita ya watani wao wa jadi, Yanga na mwishoni mwa siku wakapoteza dhidi yao.
Jumamosi,Julai 3 Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, ilijikuta ikifungwa 1-0 na Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, huku mfungaji akiwa Zawadi Mauya dakika ya 11.
Kipigo hicho kimevuruga mipango ya Simba ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara mbele ya Yanga kwani wangeshinda, basi wangetangaza ubingwa mbele ya watani wao wa jadi.
Akizungumza na Spoti Xtra, Gomes alisema kabla ya mchezo huo, alitenga muda mwingi kwa ajili ya kuangalia mbinu na aina ya uchezaji wanayotumia Yanga, hivyo ameumia kupata matokeo hayo mabaya.
Gomes alisema baada ya kupoteza mchezo huo, hivi sasa wanaweka nguvu katika michezo ya ligi iliyosalia dhidi ya Coastal Union, Azam FC na Namungo FC.
“Bado mchezo wetu wa dabi unaniuma sana baada ya matokeo mabaya tuliyoyapata, na kama kocha mimi ndiye ninayewajibika katika hili, nafahamu mashabiki wameumia sana.
“Mechi hii ilikuwa na umuhimu mkubwa kwetu, siyo jambo zuri kupoteza mechi kubwa ya namna hii ambayo ndani yake ilikuwa na rekodi nyingi bora kama tungepata ushindi.
“Baada ya kupoteza, nguvu zangu nazielekeza katika michezo ya ligi iliyo mbele yetu,” alisema Gomes.
Wakati Gomes akisema hivyo, mfungaji wa bao hilo, Mauya alisema: “Kiukweli hatukuwa na presha kwenye mechi yetu na Simba ndiyo maana tumeshinda huku tukicheza vizuri.
“Tulifanya majukumu yaleyale ambayo tunayafanya kwenye mechi nyingine na mazoezini na tuliendelea kucheza kwa kujiamini. Tunaenda kufanya hivi tena Kigoma,” .