Home Makala AZAM MEDIA MNASTAHILI PONGEZI, IKUMBUKENI NA LIGI YA WANAWAKE

AZAM MEDIA MNASTAHILI PONGEZI, IKUMBUKENI NA LIGI YA WANAWAKE



AZAM Media hivi karibuni iliingia mkataba wa kurusha maudhui ya Klabu ya Yanga, mkataba ambao utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 34.8.

Mkataba huo wa Yanga utakuwa ni wa miaka 10 na wao wametoa maelezo ni namna gani watakuwa wanailipa klabu hiyo kwa kipindi hicho chote ambacho watakuwa wakifanya kazi.

Kumbuka kuwa Azam hao kabla ya kuingia mkataba huu na Yanga tayari awali walimwaga fedha ndani ya Ligi Kuu Bara kwa kuingia mkataba wa miaka 10 na kutoa kiasi cha sh.bilioni 225.6 na mgawanyo wa fedha hizo ukawekwa wazi na utaanza kutumika msimu wa 2021/22.

Kwa hiyo mkataba huo wa Yanga ulitangazwa hivi karibuni sio wa kwanza kwa upande wa Azam Media kwa mwaka huu kwa maana hiyo ni mwendelezo katika kukuza soka letu Tanzania.

Kwa hiki ambacho wanafanya Azam Media kwa sasa wanastahili pongezi kubwa sana kwani wanalifanya soka la Tanzania kuelekea kukua kwa kiasi kikubwa jambo ambalo miaka ya nyuma halikuwepo.

Kwa sasa wachezaji wa kitanzania wataendelea kujitangaza kupitia maudhui ambayo yatakuwa yanarushwa na wadhamini wao hao.

Na klabu msimu ujao zitapambana kwa bidii sababu katika mchanganuo wa fedha hizo kwa msimu ujao kila mmoja anapata fedha kutokana na nafasi ambazo watamaliza ndani ya ligi hiyo.

Pia kitu ambacho anafanya sasa Azam sio cha kubezwa hata kidogo kwani wao wanabaki kuwa mfano kwa kuigwa kwa makampuni mengi kuhakikisha nao wao wanajitoa katika kusapoti na kukuza soka la Tanzania kwa kujitolea udhamini wa ligi pamoja na klabu ambazo zinashiriki ligi tofauti hapa nyumbani.

Ninaamini huu ni mwanzo tu kwa upande wa Azam Media katika kuzidi kulisapoti soka la Tanzania tunaamini mengi yatakuja kwao cha msingi tuendelee kuwaunga mkono kwa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Wakati tayari wamejitoa kusapoti soka la Tanzania na Klabu ya Yanga natamani kuona Azam Media pia inahamia kwenye Soka la Wanawake ambalo kwa sasa ni wazi limeanza kupiga hatua.

SOMA NA HII  BAADA YA KUHAMIA YANGA NA KURUSHA VIJEMBE SIMBA...WANASAIKOLOJIA WAMTABIRIA HAYA MANARA

Natamani kuona siku moja Ligi Kuu ya Wanawake kwa kuanzia hapo inaonekana katika runinga au kwa kupata udhamini mnono ambao utazidi kutoa hamasa wanawake kuendelea kufanya vizuri kwenye soka hasa katika levo ya timu ya taifa.

Kwa sasa upande wa wanawake mambo yanaonekana mazuri licha ya ligi hiyo kutokuwa na wadhamini lakini wamekuwa wakipambana kufanya vizuri japo wamekuwa wakipata changamoto kadhaa kama za timu kushindwa kusafiri na hata kupelekea baadhi yao kushushwa daraja kutokana na kukosa fedha hili naamini litapita endapo watapata udhamini.


Wanawake ninaamini wanaweza zaidi wanahitaji sapoti kwa kiasi kikubwa kwa kuhakikisha timu zao zinafanya vizuri na kuepukana na changamoto za hapa na pale.

Hongera Azam Media kwa kazi nzuri tunaamini mtaendelea kujitoa katika soka la Tanzania.


Mwandishi ni Martha Mboma